Mtwara. Wakati Serikali ikiendelea kuwakumbusha wananchi kuwa Juni Mosi, 2019 ndio mwisho wa matumizi ya mifuko ya plastiki, Shirika la Kuhudumia Viwanda vidogo (Sido) Mkoa wa Mtwara limeanza kutoa mafunzo ya kutengeneza mifuko mbadala kwa wajasiriamali.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Mei 21, 2019 na kaimu meneja wa Sido mkoani Mtwara, Zamla Dongwala wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara kuhusu uandishi wa habari za sayansi, teknolojia na utafiti yaliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia.
Amesema ili kutekeleza agizo la Serikali wameanza kutoa elimu hiyo ili kupata mifuko mbadala na kwamba tayari baadhi ya wajasiriamali wameonyesha nia ya kutaka kujifunza.
“Katazo la mifuko ya plastiki ni fursa kwa wajasiriamali wadogo na wameanza kuja kwenye kituo chetu kutaka kufahamu ni kwa namna gani wataweza kutengeneza mifuko mbadala lakini pia na wao watalazimika kuitumia katika shughuli zao,” amesema Dongwala
Mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia, Dk Bakari Msangi amesema ili kulinda mazingira watengenezaji wa mifuko ya plastiki wana wajibu wa kubuni na kutengeneza vifungashio mbadala kama vile vya karatasi na vifungashio vitokanavyo na mimea kama vikapu.
“Ni wajibu wa wale wenye viwanda vya mifuko ya plastiki kubuni teknolojia mbadala itakayokuja na vifunganishio vinavyooza vikianguka ardhini na visivyochafua mazingira,” amesema Dk Msangi
Pia Soma
- Mbunge CUF adai akimsalimu Waziri Mpina hamjibu
- Mongella: Ajali ya Mv Bukoba ni kumbukumbu mbaya yenye funzo
- Sweden kuendeleza misaada ya uwezeshaji wa kisheria LHRC