Dampo la Pugu ni eneo maarufu kwa kukusanya taka zote zinazozalishwa na wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam. Ukisogea karibu na eneo hilo utahisi harufu kali na wakati mwingine moshi unaotoka katika taka zilizohifadhiwa katika dampo hilo.
Mbali na hivyo pia barabara za kuelekea ndani ya dampo hazipitiki vizuri kutokana kulundikana kwa takataka katika barabara hizo.
Mbali na harufu na moshi huo, bado kuna watu wanaofanya shughuli za kujipatia kipato ndani ya dampo hilo wakiwamo mama lishe na wakusanya baadhi ya vitu vilivyotupwa jalalani hapo.
Vilevile pembeni ya dampo hilo kuna shule na hospitali ambazo kwa mujibu wa daktari wa hospitali hiyo majengo hayo yalikuwapo kabla ya kuanzishwa kwa dampo hilo.
daktari wa zahanati hiyo ya Ananda Marga, Norbetus Byase anasema changamoto zinazowakumba wao kuwa karibu na dampo hilo ni mazingira yasiyo rafiki kwa wagonjwa na watoa huduma, vitendo vya wizi na barabara mbovu hali inayofanya wagonjwa kupata tabu kuifikia hospitali hiyo.
“Barabara ya kupita kuja huku imefunikwa na takataka hali inayosababisha wagonjwa kushindwa kupita kuja kupata huduma hasa katika kipindi cha mvua,”anasema.
Anasema kipindi cha mvua hali ndio huwa mbaya zaidi kwakuwa maji hufika hadi ndani, moshi na harufu inayotoka kwenye dampo hilo inawaweka katika hatari ya kupata maradhi ya mlipuko na mfumo wa upumuaji.
“Mida ya jioni kuna moshi mzito unaotoka huko dampo kuja huku hali inayofanya tunashindwa kuendelea kutoa huduma ya matibabu na kutulazimu kurudi nyumbani,”alisema.
Alisema mbali na changamoto hizo lakini pia baadhi ya wezi hujificha katika dampo hilo kisha ifikapo usiku hufanya matukio ya wizi.
“Tunaibiwa sana vifaa vya hapa hospitali na vijana hao, tuliwahi ibiwa hadi pampu inayotusaidia kusambaza umeme katika hospitali hii na kutugharimu Sh2 milioni.
Mwalimu wa shule ya awali ya Ananda Marga, iliyopo jirani na eneo hilo, Theresia Lazaro anasema changamoto za dampo hilo zikiwamo harufu na kujaa kwa maji kipindi cha mvua kumesabisha kupungua kwa idadi ya wanafunzi wanaopelekwa kusoma katika shule hiyo.
“Awali tulikuwa tunapokea wanafunzi hadi 70 lakini sasa nina wanafunzi 30 tu, kutokana na mazingira kutokuwa rafiki mfano harufu na nzi wengi waliopo eneo hili hufanya wanafunzi kutosoma kwa uhuru muda mwingine hutulazimu kufunga hata madirisha,”alisema.
Mmoja wa wakazi wa karibu kabisa na eneo hilo Yunis Elias alisema harufu kali na moshi mzito unaotoka katika dampo hilo unasababisha wakazi wa karibu na eneo hilo kusumbuliwa na vifuahaswa kwa watoto wadogo.
“Yani mida ya jioni baada ya magari mengi kutupa taka au taka zinaporipuka hutokea moshi mzito unaoambatana na harufu kali inawafanya watoto wetu kuugua vifua, mwanangu haipiti mwezi bila kuugua,” anasema.
Pia mkazi mwingine wa eneo hilo, Abdallah Hassan anaeleza kuwa katika kipindi cha mvua kubwa hali ya moshi hupungua lakini harufu huzidi katika kipindi hicho.
“Yaani changamoto tunazopata na dampo hili hazina mvua wala jua ni kutaabika tu,”alisema.