Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shule za msingi 500, sekondari 185, vyuo vikuu 5 vyajengwa Iringa

Bf2ed7ffe8f58d6bad7e9b221d93f241.jpeg Shule za msingi 500, sekondari 185, vyuo vikuu 5 vyajengwa Iringa

Mon, 6 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Shule za msingi zaidi ya 500, sekondari 185 na vyuo vikuu vitano ni sehemu ya mafanikio makubwa katika sekta ya elimu ambayo mkoa wa Iringa unajivunia ndani ya miaka 60 ya uhuru.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga aliyasema hayo wakati akifungua Kongamano la Miaka 60 ya Uhuru, mjini hapa. “Haya ni mafanikio makubwa katika sekta hii yaliyokwenda sambamba na mafanikio katika sekta nyingine nyingi za maendeleo mkoani kwetu,” alisema.

Kongamano hilo lilifanyika kwa uratibu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa, Chuo Kikuu Huria na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).

Mkuu huyo wa mkoa alisema pamoja na mafanikio makubwa katika sekta ya elimu, idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya mkoani humo nayo imeongezeka kutoka tisa hadi 292 sambamba na mafanikio mengine katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwamo maji, barabara, mawasiliano, utalii, biashara, kilimo, viwanda na mazingira.

“Kama mnavyofahamu mwaka huu tunaadhimisha miaka 60 ya uhuru. Katika kipindi hicho tumepiga hatua za maendeleo katika nyanja zote hivyo tunapaswa kujivunia mafanikio haya,” alisema. Alisema ndani ya miaka hiyo, Tanzania imeendelea kuwa nchi na taifa huru, imara na lenye umoja, mshikamano, amani na utulivu na kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Alisema kuzidi kuimarika kwa sekta ya elimu kuna ufanya mkoa huo na taifa kuwa na nguvu kazi inayojitambua na yenye uwezo wa kutumia rasilimali zinazowazunguka kujiletea maendeleo. “Kwa kupitia kongamao hili la miaka 60 ya uhuru, ni matarajio yetu kwamba mtakuja na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mitaala yetu ya elimu ili kuakisi ubora wa elimu inayotolewa,” alisema.

Sendiga alisema wakati huu ambapo serikali inafanya jitihada za kukuza uchumi wa kati unaotegemea maendeleo ya viwanda, ni lazima kupatikane wataalamu wengi watakaosaidia kuendesha viwanda hivyo. Alisema serikali imeendelea kufanya mabadiliko kadhaa katika mitaala yake ya elimu ili kuwezesha kutolewa kwa elimu bora inayomjengea mwanafunzi ujuzi.

Katika kongamano hilo, wasomi, wadau na viongozi mbalimbali walikubaliana kwamba ili uchumi wa kati unaotegemea viwanda uwezo kufikia malengo yake, ni lazima kuhakikisha elimu inayotolewa ni ile inayowawezesha wahitimu kujitegemea.

“Tanzania haiwezi kufikia azma yake hiyo kama haitawezesha wananchi kupata elimu itakayowawezesha kujitegemea na kuendana na mahitaji ya soko la ajira nchini na duniani kwa ujumla,” alisema Mkuu wa Wilaya Mstaafu, Pascal Mhongole.

Chanzo: www.habarileo.co.tz