Mkuu wa mkoa wa Njombe, Antony Mtaka ameziagiza halmashauri mkoani humo kutumia wataalamu wake wa TEHAMA kufanya tathmini ya ufungaji wa kamera za ulinzi (CCTV Camera) katika shule za sekondari za bweni kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na kulinda maadili.
Mtaka ametoa agizo hilo alipokuwa akikagua hali ya Wanafunzi wa kidato cha tano kuripoti katika shule za sekondari walizopangiwa pamoja na kukagua ujenzi wa miundombinu ya mabweni, madarasa na vyoo kwa ajili ya Wanafunzi hao.
Amesema kutokana na kukithiri kwa vitendo vya uvunjifu wa maadili kwa watoto na vijana ambapo shule za bweni zimekuwa hatarini zaidi, ni lazima zifungwe kamera ili kupambana na vitendo hivyo.
Aidha, Mtaka amesema kamera hizo pia zitasaidia kudhibiti matukio ya moto ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika shule za bweni.