Dar es Salaam. Ikiwa imebaki siku mbili, wanafunzi wa darasa la saba nchini Tanzania kufanya mtihani wa taifa, Shule za Atlas nchini humo zimefanya maombezi kwa ajili ya wanafunzi wake watakaofanya mtihani huo.
Maombi hayo yaliyoshirikisha uongozi, walimu, wazazi na wanafunzi yalifanyika jana Jumapili Septemba 8, 2019 katika shule hizo zilizopo Ubungo na Madale wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika maombi hayo, Mkuu wa shule ya Atlas Ubungo, Justus Kagya alisema wameamua kufanya jambo hilo kama njia ya kumkabidhi Mungu watoto hao waweze kufanya vizuri katika mitihani hiyo.
“Sisi kama walimu tumetimiza wajibu wetu kwa ailimia 100, kilichobaki ni kumkabidhi Mungu aweze kutenda na watoto wetu wafaulu vizuri mitihani hiyo ya taifa,” alisema Kagya.
Kuhusu matokeo ya shule, alisema kwa mwaka 2016 na 2017 shule hiyo ilishashika nafasi ya kumi bora kitaifa hivyo wana imani hata mwaka huu itafanya vizuri.
Wakati kwa idadi ya watoto wanaotarajiwa kumaliza amesema wapo 248 kati yao wanaume ni 124 na wanawake 124.
Pia Soma
- Kada CCM avamiwa, acharangwa mapanga Dar
- Wanafunzi 11,200 kufanya mtihani darasa la saba Arusha, watamba kufanya vizuri
- VIDEO: Mmiliki wa baa Dar abanwa na Waziri Lugola, aishiwa nguvu
Kwa upande wao wanafunzi akiwemo Neila Mbugunde alisema kwa maombi yaliyofanyika wana imani watafanya vizuri ukizingatia hadi wazazi wao wameshiriki ipasavyo na kuongeza kuwa hata maandalizi ya darasani yalikuwa mazuri.
Mary Ipembe ambaye ni mmoja wa wazazi alisema maombi ni kitu kizuri katika maisha ya kila siku na kwa wanafunzi nao bila maombi shetani anaweza kuwapitia na kujikuta wanafanya vibaya.
Ipembe alisema kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia maendeleo ya mtoto wake na ufundishaji wa shule hiyo wanaamini watafaulu vizuri.