Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shule yenye wanafunzi 1500 haina choo Chato

Choo Shuleeeee.png Shule yenye wanafunzi 1500 haina choo Chato

Wed, 14 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ukistaajabu ya Mussa, subiri kuona ya Firauni. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya yo Shule ya Msingi Ludeba iliyopo wilayani Chato mkoani Geita yenye wanafunzi zaidi ya 1500, kuwa haina tundu hata moja la choo.

Hali hiyo inawafanya wanafunzi kujisaidia vichakani na kusababisha utoro.

Mbali na ukosefu wa vyoo pia shule hiyo inakabiliwa na uchakavu na uchache wa miundombinu ya vyumba madarasa, nyumba za walimu hali inayowalazimu kuishi wilaya jirani ya Bukombe.

Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Deusdedith Katwale aliyetembelea na kujionea mazingira yalivyo shuleni hapo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Daud William amesema ilijengwa mwaka 1999 na haina hata tundu moja la choo.

Mkuu wa Wilaya ya Chato, Deusdedith Katwale akitembelea Shule ya Msingi Ludeba ambayo ina wanafunzi 1500 ikiwa haina hata tundu moja la choo. Picha na Rehema Matowo

“Ujio wako Mkuu wa Wilaya utakua mwarobaini wa matatizo ya shule hii tuna watoto 1500 haina hata tundu moja la choo kilichokuwepo kilijaa zaidi ya miaka minne iliyopita, naomba tutakuonyesha ujionee mwenyewe.”

“Fedha za ukarabati ninazopata nimechimba shimo lakini nimeshindwa kumalizia, watoto hawahudhurii shule hasa wa kike maradhi ya kila mara yanatokea ukifika utatoa machozi naomba usiishie ofisini fika ujionee,”amesema

Changamoto nyingine ni uhaba wa nyumba za walimu na wanazoishi ni kama magofu ambayo yanatunza nyoka na hazina vyoo imara, na vilivyopo vimejengwa kwa matete ya nyasi na kuhatarisha usalama wao.

“Tuko walimu 13 kuna nyumba kama gofu ukiingia unakutana na nyoka vyoo ni vya matete kama ni kijana wako yuko pale kazi anaacha, lakini walimu hawa hawana namna wanafanya kazi kwenye mazingira magumu.”

Amesema kutokana na eneo hilo kutokuwa na nyumba za kupangisha walimu wamelazimika kwenda kupanga wilaya jirani ya Bukombe, na ili kuja shule wanalazimika kuvuka mto ambao una maji mengi hivyo kulazimika kubeba nguo mbili ili asiingie darasani akiwa ameloa na wakati mwingine hulazimika kuvushwa kwa mtumbwi au kubebwa mabegani, hivyo kushusha kiwango cha taaluma shuleni.

Kutokana na hali hiyo Katwale alilazimika kumpigia simu Mkurugenzi wa halmashauri ya Chato kutaka kujua ipi mipango ya halmashauri hiyo kuhakikisha mazingira ya shule hiyo yanaboreshwa.

Akizungumza kwa simu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chato, Mandia Kihiyo amesema shule hiyo ipo kwenye bajeti na tayari imepata mfadhili Hellen Foundation atakayejenga vyoo.

Kuhusu madarasa amesema haikuwa kwenye bajeti, lakini wanafanya mchakato kuona namna gani ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia shuleni hapo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live