Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shule yenye madarasa mawili inavyopambana kujinasua na changamoto

52914 SHULE+PIC

Thu, 18 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nanyumbu. Mara nyingi yanapotokea matokeo mabaya ya mitihani kwa wanafunzi lawama huelekezwa sehemu mbalimbali ikiwamo kwa walimu, lakini sababu zipo nyingi zinazoweza kuwa kikwazo cha kufikia malengo ya kupatikana kwa elimu bora na shule kutofanya vyema.

Moja ya sababu hizo ni uchache wa miundombinu, upungufu wa walimu, mazingira duni ya kufundisha na kujifunzia na mwamko mdogo kwa baadhi ya wazazi na jamii inayozunguuka mazingira ya shule husika. Mila na desturi pia ni sababu zinazotajwa kuchangia baadhi ya maeneo kutofanya vizuri huku suala la mimba kwa wanafunzi nalo likiwa katika orodha ya changamoto.

Miongoni mwa shule zenye changamoto ni Shule ya Msingi Mehiru ya wilayani Nanyumbu Mkoa wa Mtwara yenye wanafunzi 172 wa kuanzia darasa la awali hadi la saba, ikiwa na vyumba viwili pekee vya madarasa, matundu sita ya choo, matatu ya wavulana yakiwa yameezuliwa paa.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Fabian Frank anasema kutokana na shule hiyo kuwa na vyumba viwili tu vya madarasa wanafunzi wa darasa la tatu na la nne hulazimika kusomea katika madarasa yasiyo rafiki kutokana na hali halisi.

Madarasa hayo ni ya miti yaliyokandikwa kwa udongo lakini uimara wake ni hafifu kwani yameezekwa kwa nyasi na wakati wa mvua huwa na hali mbaya kutokana na kupitisha maji ambayo huwalowesha waliomo ndani.

Wanafunzi wa darasa la tano, sita na saba hulazimika kusomea kwenye chumba kimoja huku wa darasa la awali, la kwanza na pili wakisomea kwenye chumba kingine.

“Tumepanga ratiba ya masomo lakini tunashindwa kuifuata kwa sababu mwalimu mmoja akiingia kufundisha inabidi mwingine asubiri hadi amalize mwenzake ndipo na yeye aingie, kwa hiyo ratiba kuu ya masomo haifuatwi inavyotakiwa,” anasema Mwalimu Frank.

Anasema kwa sasa shule hiyo ina walimu wanne lakini mahitaji ni walimu saba kutokana na idadi ya masomo.

Mwalimu wa nidhamu, Mohamed Chilapile anasema kitendo cha chumba kimoja cha darasa kukaa wanafunzi wa madarasa matatu, huwakosesha wanafunzi fursa ya kufundishwa masomo yote kwa wakati.

“Kipindi cha kwanza kinaanza saa 2:00 asubuhi hadi saa 2:40 athari iliyopo madarasa matatu yanakaa chumba kimoja kwa hiyo kipindi kimoja cha asubuhi wanasoma darasa moja na kipindi kinachofuata ni hivyo hivyo, hadi kufikia saa 9:20 walimu vipindi vyetu vinakuwa havitimii na watoto hawapati elimu kama inavyotakiwa,” anasema Mwalimu Chilapile.

Ukosefu wa nyumba za walimu

Mwalimu Frank anasema kwa sasa shule hiyo ina nyumba mbili za walimu, hivyo kuwalazimu kuishi kwa kugawana chumba kimoja kimoja na kuchangia sebule.

“Mimi na mwalimu mwenzangu tunakaa nyumba moja. Kila mmoja ana familia yake kwa maana hiyo tunatazamana milango, halafu mwalimu mwingine amepata chumba mtaani ambacho anaishi na mazingira yake sio mazuri,” anasema.

Mwalimu Sharifu Joseph anasema kukosekana kwa nyumba za kutosha za walimu kunamfanya akae mbali na shule na ambako mazingira yake sio mazuri.

“Wananchi wana maisha yao ni tofauti kidogo na yale ya mwalimu ambaye anatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kitabia na kimwenendo,” anasema

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mehiru, Andrea Suluhu anasema wananchi walijitolea na kujenga vyumba viwili vya madarasa lakini wamekwama kutokana na hali ya uchumi.

“Tunaomba Serikali itusaidie tumalizie madarasa kwa sababu sisi wenyewe tulishaanza kuifanya hiyo kazi lakini tumekwama fedha ya kununulia saruji, misumari na mabati ili tuendelee na ujenzi,” anasema.

Kuhusu suala la walimu anasema mara kwa mara amekuwa akitembelea shuleni hapo kama kingozi wa kitongoji kuona hali ilivyo na huwakuta walimu wakiwajibika licha ya changamoto zilizopo.

Ofisa elimu msingi wilaya ya Nanyumbu, Hamis Milowe anakiri kuwepo baadhi ya shule zenye vyumba viwili au vitatu vinavyotumika kuanzia darasa la awali hadi la saba na kulazimika madarasa tofauti kusomea katika chumba kimoja.

“Mahitaji yetu ni vyumba 881 vya madarasa, vilivyopo ni 411 hivyo tuna upungufu wa vyumba 470. Tangu kampeni ya ujenzi wa madarasa ilipoanzishwa mwaka 2017 tuna vyumba vya madarasa mapya yanayoendele kujengwa 146,” anasema Milowe.

Kuhusu nyumba za walimu anasema mahitaji ni nyumba 1,036, zilizopo ni 386 na pungufu ni 650 huku vyoo mahitaji ni matundu 1,879, yaliyopo ni 706 na pungufu ni 1,170.

“Kwa sasa nyumba za walimu 476 ziko katika hatua mbalimbali sambamba na matundu 20 ya vyoo vya walimu, Serikali bado tunaendelea na jitihada kutatua changamoto zote zinazoikabili elimu katika wilaya ya Nanyumbu,” anasema Milowe.



Chanzo: mwananchi.co.tz