Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shule yazidiwa, wanafunzi wasomea kanisani

F93b038b59885df29341c35aeaaa51e0.jpeg Shule yazidiwa, wanafunzi wasomea kanisani

Wed, 9 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WANAFUNZI wanaosoma darasa la nne na la tano katika Shule ya Msingi Filimule iliyopo katika Kata ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi wamelazimika kusomea ndani ya jengo la Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda kwa zamu kutokana na ukosefu wa vyumba vya madarasa.

Sambamba na hao, wanafunzi wa madarasa mengine nao wanalazimika kusoma nje wakiwa wameketi chini.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Filimuke, Morad Wenati amekiri kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa shuleni hapo.

Alisema mahitaji halisi ya vyumba vya madarasa ni 18 huku vilivyopo ni vinane hivyo upungufu ukiwa vyumba kumi.

Akizungumzia changamoto hiyo, mwanafunzi Oliver Matosha alisema kusomea nje kunasababisha utoro kwa wanafunzi hususani msimu huu wa mvua za masika.

Naye mwanafunzi Cecilia James alisema katika kipindi hiki cha mvua walimu wao wanalazimika kusitisha kufundisha pindi mvua zinaponyesha.

"Hili jengo la kanisa ambalo tunalitumia kama darasa tunapokezana kati ya wanafunzi wa darasa la nne na la tano.

Tunatumia mabenchi ya kanisa yanayokaliwa na waumini lakini shida iliyopo tunashindwa kuandika vizuri, siku za ibada wanalitumia jengo lao,"alieleza Cecilia.

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Nsimbo, Mohamed Ramadhani amekiri kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa kwamba tangu isajiliwe miaka saba iliyopita ina vyumba vinne.

“Ila vyumba vitatu vimejengwa kwa michango ya wananchi na wadau na ujenzi umefikia linta na katika mwaka huu wa fedha zimetengwa fedha kumalizia,”alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz