Shule ya Msingi Kiziba iliyopo Kijiji cha Mwenegeza wilaya na mkoa wa Geita inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi kukaa chini.
Shule hiyo yenye wanafunzi 874 ilianza mwaka 2018 na kwa sasa ina madarasa sita hivyo kusababisha wanafunzi zaidi ya 140 kutumia chumba kimoja cha darasa.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Beatus Mwandu aliyasema hayo wakati wa hafla ya kupokea vyumba viwili vya madarasa vilivyojengwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML).
Alisema shule hiyo inahitaji vyumba vya madarasa 17 na kwamba mbali na upungufu wa madarasa pia ina uhuba wa nyumba za walimu na madawati na kuomba wadau kusaidia ili wanafunzi waweze kusoma kwenye mazingira rafiki.
“Kushukuru ndio kuomba tena hapa changamoto bado ni kubwa madarasa yako kwenye hali mbaya hayana sakafu, milango, madirisha wala ripu kwa kweli hali ni tete na ukiweka na kukosa madawati mtoto anakaa kwenye vumbi ni hali mbaya hata sisi walimu tunajisikia wanyonge matumaini yangu mtaendelea kutushika mkono,” alisema
Mwalimu Mwandu alisema shule hiyo ina madawati 160 ambayo hayatoshelezi kuendana na sera ya elimu ya wanafunzi watatu dawati moja hivyo kuwa na uhitaji wa madawati 126,na atundu ya vyoo 23 na kwamba kwa sasa yaliyopo ni tisa yanayotumiwa na wanafunzi 874.
Madarasa hayo yaliyogharimu Sh42 milioni yalikabidhiwa na Afisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Dorine Denis kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa GGML, Terry Strong ambapo alisema elimu ni nguzo muhimu ya jamii hivyo bila elimu ni vigumu kupata maendeleo.
“Kijiji hiki ni miongoni mwa vijiji vinavyozunguka mgodi na sisi kama mgodi tutaendelea kuwasaidia ili wapate miundombinu mizuri kwenye sekta ya elimu, afya na sekta nyingine,” alisema Denice
Alisema elimu inaweza kubadilisha maisha ya watu na ni mwelekeo wa miradi yetu ya uwekezaji wa jamii.
“GGML inaamini wananchi wa Tanzania ndio mtaji mkubwa wa kampuni hii na siku zote imekuwa ikiunga mkono juhudi za serikali za kuboresha elimu na kujenga kizazi kijacho ambacho kitasaidia taifa la Tanzania kufikia malengo yake makubwa ya kiuchumi na kimaendeleo,” alisema
“Tumedhamiria kuchochea maendeleo endelevu ya jamii zinazozunguka mgodi na imedhihirisha hilo mara kwa mara kwa kushirikiana kikamilifu na Serikali katika kuboresha huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, maji na barabara pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi kwa jamii zinazozunguka mgodi huo.
Kwa upande wake, Afisa elimu msingi wa Halmashauri ya Geita, Edith Mpinzile alikiri shule hiyo kuwa na changamoto mbalimbali na kwamba katika kukabiliana nazo kwa mwaka huu wamelenga kuchonga madawati 100 na kujenga matundu matano ya vyoo kwa kutumia fedha za uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).
Pia, alisema kupitia Mradi wa kuboresha upatikanaji wa fursa katika utunzaji bora wa elimu ya wali na msingi Tanzania bara (Boost) watajenga vyumba vitano vya mdarasa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani.
Naye Mtendaji wa Kata ya Nyakagomba, Christopha Amos naye aliishukuru GGML kwa msaada huo na kuahidi kufikisha kilio cha changamoto nyingine kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili azifanyie kazi.