Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shule ya Msingi Majimatitu kugawanywa

Tue, 4 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Serikali imeanza utaratibu wa kujenga shule nyingine ya msingi ili kugawanya Shule ya Msingi Majimatitu iliyopo Mbagala jijini Dar es Salaam ambayo ina wanafunzi zaidi 4,000.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Septemba 4, 2018 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kuteuliwa (CCM) Salma Kikwete.

Katika swali lake la nyongeza, Salma ambaye ni mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema shule hiyo ina wanafunzi 4,000 na kuhoji kuna mkakati gani wa haraka kuhakikisha inaongezewa madarasa.

Akijibu swali hilo, Jafo amesema mwaka jana shule hiyo ilidahili wanafunzi 1,200 wa darasa la kwanza hali iliyosababishwa na sera ya elimu bure kwa shule za msingi hadi sekondari.

Hata hivyo, amesema Serikali imetafuta eneo jingine kwa ajili ya ujenzi wa shule pacha ili kuigawanya shule hiyo.

“Tunafanya haraka iwezekanavyo ili shule hiyo ikamilike haraka tupunguze idadi ya watoto katika shule hiyo,”amesema.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum (CUF) Sonia Magogo amehoji Serikali inasaidiaje watoto wa shule ya msingi wilayani Handeni ambao wamekuwa wakisongamana kwenye darasa moja.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Tamisemi, Joseph Kakunda amesema ongezeko la wanafunzi katika shule za msingi na sekondari ni moja ya changamoto iliyotokana na utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo.

“Katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali ilikamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa sita kwa kiasi cha sh 40.96milioni katika shule za msingi Kwazala, Ugweno na Gumba,”amesema.

Amesema pia Mbunge wa Handeni kupitia fedha za mfuko wa jimbo alikamilisha ujenzi wa madarasa saba kwa gharama ya sh 37.63 milioni katika Shule za Kabuki Mjini, Gole, Mnyuzi na Msilwa.

“Serikali itaendelea kujenga miundombinu ya elimu katika halmashauri ya Handeni na inawaomba wananchi na wadau kushiriki kikamilifu katika juhudi za kupunguza tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa,”amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz