Dar es Salaam. Shule ya Kimataifa ya Kifaransa, iliyopo Masaki Jijini Dar es Salaam imetoa fursa kwa wazazi na walezi nchini Tanzania kunufaika na punguzo la robo tatu ya ada kwa wanafunzi watakaoanza masomo katika shule hiyo na baadaye vibali vya kusoma vyuo nchini Ufaransa kwa gharama nafuu.
Kwa mujibu wa uongozi wa shule hiyo maarufu, French School Arthur Rimbaund, mzazi atalazimika kukubaliana na mfumo wa elimu ya Kifaransa, utakaofundishwa kwa lugha ya Kifaransa, ukihusisha masomo saba (sekondari), matano (shule ya msingi) na matatu (chekechea).
Bernadette Mande ambaye ni mratibu wa Michezo wa Shule hiyo iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam amesema leo Ijumaa Juni 21, 2019 kuwa Watanzania wananufaika na fursa hiyo. Aidha, shule ina wanafunzi 330 ikitumia mbinu mbalimbali za michezo katika ufundishaji.
“Watanzania na Wafaransa wana ada yao tofauti, wanalipa less than 25 percent ya ada, hii ni makubaliano ya Ufaransa na Tanzania, lakini mataifa mengine wanalipa ada kama ilivyo,” amesema Bernadette wakati wa ziara ya wanahabari katika Kampasi mpya ya Shule hiyo eneo la Masaki, Jijini Dar es Salaam.
Akifafanua kuhusu ada hizo, Benardette amesema ada za shuleni hapo ni euro 5,000 hadi 5,500 kwa chekechea, euro 6,000 hadi 7,000 kwa ngazi ya shule ya msingi na euro 7,000 hadi 9,000 kwa kidato cha kwanza hadi cha sita.
Kwa mujibu wa takwimu za maduka ya kubadilishia fedha, mzazi atakayempeleka mwanaye kuanza masomo katika shule hiyo mwaka 2019 atalazimika kulipia kati ya Sh3.1milioni hadi Sh3.4 milioni badala ya Sh12.5 milioni hadi Sh13.8 milioni kwa ngazi ya chekechea.
Pia Soma
- Serikali yafungua mnada wa kimataifa wa mifugo Longido
- Jaji Mkuu Zanzibar awapa somo majaji, mahakimu
- VIDEO: Bwana harusi aanguka wakati wa kumuaga bibi harusi aliyekufa ajalini Mbeya
“Mtanzania akishamaliza kidato cha sita shuleni hapo, atapatiwa kibali na Ubalozi wa Ufaransa kusoma chuo chochote nchini Ufaransa kwa gharama zitakazokuwa na unafuu zaidi ikilinganishwa na gharama ambazo angelipia kwa hapa Tanzania,” amesema Bernadette.
Katibu wa Bodi ya Uendeshaji wa Shule, Rajabu Katunda amesema Shule hiyo inajumuisha zaidi ya wanafunzi waliotoka mataifa 40 duniani, waishio hapa nchini Tanzania, wakisoma mitalaa ya mfumo wa Kifaransa unaokubalika katika mifumo mingine ya elimu duniani.