Serengeti. Shule nane za msingi wilayani Serengeti zimepewa vibali vya kusajili wanafunzi wa awali na darasa la kwanza.
Kutolewa kwa vibali hivyo kunaifanya wilaya hiyo yenye vijiji 78 kuwa na shule 122 za msingi za Serikali kutoka 114 za awali.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Januari 21, 2020 mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Juma Hamsini amesema kusajiliwa kwa shule hizo kutaleta mafanikio ya kitaaluma kwa watoto.
"Kazi tunayopambana nayo kwa kushirikiana na wazazi ni ukamilishaji wa miundo mbinu ili tuweze kukidhi vigezo na kuandikisha wanafunzi wa awali na darasa la kwanza kwa mkondo mmoja," amesema.
Amezitaja shule zilizopata usajili kuwa ni Makorobio, Manyago, Michuri, Maliwa, Kichongo, Nyamihuru, Bukore na Gwikongo.
Amebainisha kuwa shule hizo zitapangiwa walimu wengi ili kuendana na wanafunzi waliopo.
Pia Soma
- Kampuni ya Green Miles yatia ngumu kuachia kitalu
- TCU yavifutia usajili vyuo tisa Tanzania
- Wamiliki wa mabasi waliotuhumiwa na DC Sabaya wajisalimisha polisi