Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shule aliyosoma Mwalimu Nyerere kukarabatiwa

Shule aliyosoma Mwalimu Nyerere kukarabatiwa

Thu, 12 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serikali ya Tanzania  imeamua kuifanyia ukarabati mkubwa shule ya msingi Mwisenge ambayo alisoma Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ili iwe sehemu ya historia ya taifa hilo.

Akizungumza baada ya kutembelea shule hiyo jana (Jumamosi, Desemba 7, 2019), Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeamua kuifanya shule hiyo iliyopo kwenye manispaa ya Musoma iwe sehemu ya historia ya Mwalimu Nyerere pamoja na historia ya Tanzania kwa ujumla.

“Shule hiyo haiwezi kubeba historia ya Mwalimu Nyerere, endapo majengo na miundombinu ya shule hiyo haitakarabatiwa na kujengwa upya. Mipango ya kuifanya shule hiyo iwe sehemu ya historia ya Tanzania inaendelea serikalini; na kwamba historia ya Baba wa Taifa itapatikana shuleni hapo.” 

Amesema baada ya mchakato huo kukamilika, shule ya msingi Mwisenge itaubeba mkoa wa Mara na nchi ya Tanzania kwa ujumla.

Amesema uamuzi wa kuifanya shule hiyo kuwa yenye historia ya Tanzania unatokana na viongozi mbalimbali nchini kusomea shuleni hapo wakiwamo, Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Jaji Joseph Warioba na Joseph Butiku.

Waziri mkuu pia amewapongeza viongozi wa mkoa wa Mara kwa kusimamia matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya shule hiyo na akawataka viongozi wengine wa umma waige mfano huo.

Akitoa  taarifa ya ukarabati wa shule hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma, Fidelica Myovela amesema kuwa manispaa yake inahitaji zaidi ya Sh161 milioni ili kukamilisha ukarabati huo ambao tayari umeanza.

Amesema kuwa hadi sasa wamepokea zaidi ya Sh772.6 milioni kutoka Tamisemi kwa ajili ya ukarabati huo ambapo hadi sasa wamekwishafanya ukarabati kwa asilimia 85 ya kazi yote.

Amesema kuwa kati ya fedha hizo, jumla ya Sh20 milioni  zilitolewa Septemba mwaka jana  na Rais John Magufuli ambaye pia aliagiza tathmini ya gharama za ujenzi na ukarabati wa miundombinu shuleni hapo ianze mara moja.

Chanzo: mwananchi.co.tz