Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shughuli za kibinadamu zinavyoharibu bwawa la Mindu

42645 Pic+mindu Shughuli za kibinadamu zinavyoharibu bwawa la Mindu

Tue, 19 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unapozungumzia maji mkoani Morogoro huwezi kulikwepa bwawa la Mindu ambalo linachangia asilimia 80 ya maji yanayotumika katika mkoa huo, tunaweza kusema ndicho chanzo kikuu cha maji kwa Morogoro.

Bwawa hili lililopo kilomita tisa kusini magharibi mwa manispaa ya Morogoro likichukua eneo la kilomita za mraba nne, lilijengwa kwa lengo la kukidhi matumizi ya maji ya nyumbani na viwandani.

Kulingana na takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, mkoa wa Morogoro ulikuwa na wakazi 315,866 idadi ambayo itakuwa imeongezeka mara dufu kwa sasa. Hawa wote matumizi yao ya maji yanategemea kwa kiasi kikubwa bwawa la Mindu.

Huenda baada ya miaka kadhaa ijayo upatikanaji wa maji safi na salama ukawa tatizo kubwa katika mkoa huo kutokana na chanzo hicho kikuu kuwekwa hatarini na shughuli za kibinadamu.

Bwawa hilo ambalo liko jirani na vijiji vya Kasanga, Mindu na Madanganya linaelezwa kuwa karibu na makazi ya watu ambayo yanahusisha nyumba 133 na mashamba 261.

Kulingana na Sheria ya Maji Na 42 ya mwaka 1974 na marekebisho yake yaliyofanyika katika Sheria ya rasilimali za maji ya mwaka 2009, shughuli za kibinadamu haziruhusiwi kufanyika ndani ya mita 500 kutoka kilipo chanzo cha maji.

Mwonekano wa sasa wa bwawa hilo sio wa kuridhisha kwani kina chake kimepungua huku katika baadhi ya sehemu likionekana kukauka.

Ofisa wa Maji wa Bonde la Wami Ruvu ambalo bwawa hilo lipo chini yake, Simon Ngonyani anasema uwepo wa makazi ya watu ndani ya mita 500 kutoka lilipo bwawa hilo unasababisha uharibifu mkubwa wa maji na kuyaondolea ubora unaostahili. Anasema kitaalamu uchafu unaotokana na binadamu kama vile mkojo na kinyesi hupunguza ubora wa maji.

“Ukienda kupima haya maji utakutana na vitu kama hivyo, tumeshafanya utafiti kwamba makazi ya watu yakiwa jirani mambo hayo huwezi kuzuia matokeo yake tujiandae kupata maji yaliyochafuliwa,” anasema.

Kando na hilo shughuli za kilimo zinazofanywa jirani na bwawa hilo nazo zinatajwa kuwa chanzo kingine cha uharibifu na uchafuzi.

Kwa mujibu wa Ngonyani, wakulima hao wengi wanajihusisha na kilimo cha kutumia mbolea ya chumvichumvi ambayo ina kemikali zisizofaa kwenye maji.

“Ukiacha mbolea wakati mwingine tope linatoka mashambani na kuingia bwawani, huu wote ni uchafuzi unaochangia maji kukosa ubora unaostahili,” anasema.

Uchimbaji na uchenjuaji wa madini katika eneo lililo jirani na bwawa hilo nao unatajwa kuwa chanzo cha uchafuzi.

Mbali na athari za kiafya, uwepo wa shughuli na watu katika eneo hilo unakwamisha upanuzi wa bwawa hilo kwa ajili ya kuongeza kina cha maji kufikia mita tano kwenda juu ikiwa ni mita 2.5 zaidi ya ilivyo sasa.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe anasisitiza kuwa wananchi kuendelea kuwepo kwenye eneo hilo si salama. Anasema wakazi wa eneo hilo walishatambuliwa na Serikali na kulipwa fidia ili kupisha hifadhi hiyo.

Kauli ya serikali

Akizungumza wakati mawaziri wanane walipotembelea bwawa hilo hivi karibuni ili kutafuta ufumbuzi wa changamoto iliyopo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliagiza kusitishwa uhamishwaji wa wananchi hao hadi pale uamuzi mwingine utakapotolewa.



Chanzo: mwananchi.co.tz