Shughuli za kibinadamu ikiwemo uchenjuaji wa madini ya dhahabu na kilimo katika mto Nikonga uliopo mkoani hapa zimesababisha maji ya mto huo kushindwa kutumika kwenye matumizi ya nyumbani na kuhatarisha uhai wa mto huo.
Mto huo pia hutitirisha maji yake katika mto Malagarasi na kisha Ziwa Tanganyika.
Kutokana na hali hiyo serikali imetoa Sh420 milioni kwa ajili ya kuuhifadhi mto huo ulioharibiwa kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa maji na uhifadhi wa mto Nikonga uliofanyika wilayani Geita juzi Mei 25, Mkuu wa idara ya ugawaji maji na utunzaji wa vyanzo vya maji kutoka bonde la ziwa Tanganyika, Odemba Kornel amesema mto huo umeharibika na sasa uko mbioni kupotea.
Amesema wachimbaji wadogo wamekuwa wakichenjua madini ya dhahabu kwenye vyanzo vya maji, huku wakulima wakilima hadi kwenye eneo la mto na kuchepusha mto kwenda kwenye mashamba yao bila kujali madhara yatakayotokea.
“Kuna shughuli za uvuvi haramu wakati maji yamepungua watu wanafunga mto na kuchota maji na kuyamwaga nje ili kuvua samaki aina ya kambale ni shughuli zinazoathiri mto na kusababisha mto kuwa wa msimu wakati ni mto unaotakiwa kuwa na maji wakati wote,” amesema Kornel.
Advertisement Ametaja mikakati ya kuhifadhi mto huo kuwa pamoja na kuunda jumuiya ya kusimamia mto ngazi ya jamii, kuweka mipaka ndani ya mita 60 zilizoainishwa kisheria na kuweka mabango ya kuwajulisha wananchi kutofanya shughuli za kibinadamu.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Geita Wilson Shimo, Ofisa Tawala wa wilaya hiyo, Fred Muhagama amewataka wananchi kulinda vyanzo vya maji ili visipotee kwakuwa utunzaji wa vyanzo utawahakikishia upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara.