Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shirika la Walter Reed latakiwa kupanua wigo

64a1e0838ba56b91a0173286a69e41e6 Shirika la Walter Reed latakiwa kupanua wigo

Sun, 7 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHIRIKA la Walter Reed limeombwa kupanua wigo wa utoaji huduma zake nchini ili kuwawezesha Watanzania wengi kunufaika nazo, hususani kuwawezesha mabinti na wanawake walio katika umri mdogo kupitia mradi wa Dreams.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayojishughulisha na masuala ya Ukimwi, kifua kikuu na dawa za kulevya, Fatma Toufiq ni miongoni mwa wadau waliotoa ushauri huo wakati kamati hiyo ilipofanya ziara katika mikoa ya Njombe, Mbeya na Songwe.

Toufiq alisema kama kamati wamevutiwa na mradi wa Dreams, ambao kwa kiasi kikubwa umewainua wasichana na wanawake wa umri mdogo, kwa kuwatoa kwenye mazingira hatarishi ya kuambukizwa magonjwa ya ngono na kuwapa ujuzi wa kutafuta riziki kwa njia nyingine, badala ya kujiuza.

“Tunawashukuriu sana wadau hawa kwa sababu wamesaidia sana kwenye masuala mbalimbali ya kimaendeleo, kwenye masuala ya afya, elimu na uchumi. Kwa ujumla wamejitahidi sana kuisaidia serikali yetu. Kuna hawa wenzetu wa Walter Reed ambao wako Nyanda za Juu Kusini wamefanya kazi nzuri..tumeona mpaka ule mpango walioutumia kuwajengea uwezo watoto wa kike waweze kujitambua..waweze kutoka kwenye mazingira hatarishi,” alisema.

Naibu Waziri wa Ofisi ya RaisTawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange alikiri umuhimu wa taasisi zisizo za kiserikali zinazotoa huduma za kijamii kuwa na mchango mkubwa na kusema ipo haja zinapokuwa na bajeti inayotosheleza, kupanua wigo wa utoaji huduma.

Dk Dugange alisema yapo mafanikio mengi yaliyotokana na taasisi binafsi, kuendesha miradi ndani ya jamii na ndiyo sababu serikali inaendelea kutoa ushirikiano na fursa kwa taasisi zinazoonesha moyo wa kushiriki katika utatuzi wa changamoto zinazoikabili jamii.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Waltereed, David Maganga alisema mpango wa kuwawezesha mabinti na wanawake walio katika umri mdogo, unalenga kulitoa kundi hilo kwenye changamoto ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutokana na tafiti nyingi kuonesha kuwa kundi hilo liko hatarini zaidi.

Baadhi ya wanufaika wa mradi wa Dreams, walikiri mradi huo kuyabadilisha maisha yao kutoka katika mazingira hatarishi kutokana na kufanya biashara ya ngono kwa ajili ya kujikidhi kimaisha hadi kufikia hatua ya kuingia kwenye ujasiriamali na kujitolea kutoa elimu kwa wenzao.

Chanzo: www.habarileo.co.tz