Watoto wawili wa familia moja wamefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye shimo la choo kinachoendelea kujengwa.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao kwa vyombo vya habari leo Jumanne April 4, 2023 imesema tukio hilo limetokea katika kijiji cha Itetemia, Manispaa ya Tabora.
Amewataja watoto waliofariki katika tukio hilo lililoacha simanzi kwa familia kuwa ni Rashid Hamis (3) na Sada Juma mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi sita.
"Watoto hao walikuwa wakicheza maeneo ya karibu na shimo la choo kinachoendelea kujengwa ndipo walipotumbukia na kufariki dunia kwa kunywa maji mengi,” amesema Kamanda Abwao
Amesema shimo hilo lilijaa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali nchini.
Kamanda Abwao amewasihi wazazi na walezi kuwa makini kwa kufuatilia mienendo ya watoto wao wanapocheza, hasa jirani na maeneo hatarishi yakiwemo mashimo na madimbwi ya maji.
Tukio hili limetokea wiki chache baada ya tukio lingine la watoto wa familia moja kufariki dunia kwa kuzama katika dimbwi la maji walipokuwa wakiogelea.