Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shigela apiga marufuku mgambo kukamata watu

72f69e52ae7f39c79d987e791b50439f Shigela apiga marufuku mgambo kukamata watu

Thu, 17 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigella amepiga marufuku askari wa akiba (mgambo) katika halmashauri zote za mkoa huo kufanya oparesheni yoyote ya kukamata watu wakiwemo wafanyabiashara wadogo na badala yake wapangiwe kwenye ulinzi wa majengo ya halmashauri na mali nyingine.

Mkuu huyo wa mkoa alitoa agizo hilo wakati mkutano wake na wafanyabiasha wadogo maarufu kama Wanachinga katika Soko Kuu la Chifu Kingalu mjini Morogoro.

Hatua hiyo ya Shigela imekuja siku chache baada ya askari mgambo wa Manispaa ya Morogoro kushutumiwa na wafanyabiashara wadogo kuwanyanyasa, kuwapiga na kuharibu bidhaa zao.

"Kuanzia leo (Juni 16) ni marufuku kwa askari mgambo kufanya oparesheni zozote ndani ya mkoa huu na hii ni kwa halmashauri zote, kazi za oparesheni zinafanywa na Jeshi la Polisi na kwa kibali changu sio vinginevyo," alisema.

Shigella aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri za wilaya za mkoa huo wawapangie kazi nyingine za ulinzi askari mgambo ikiwamo katika majengo yao na si kuwatumia kukamata wafanyabiashara wadogo.

Pia aliitaka manispaa hiyo kushusha gharama za pango la vizimba na vioksi katika Soko la Chifu Kingalu ili wafanyabiashara waweze kumudu.

Aidha, aliitaka kuandaa mikataba mipya yenye kuzingatia gharama mpya kuanzia Julai Mosi, mwaka huu na ukomo wake uwe ni miaka miwili.

Gharama za sasa katika soko hilo ni, vioksi vya chini Sh 300,000 na vimepunguzwa hadi Sh 100,000 , vioski vya ghorofani ni kutoka Sh 200,000 hadi 50,000 na vizimba kutoka Sh 20 000 hadi Sh 10,000 kwa mwezi.

"Gharama hizi zitadumu kwa muda wa miaka miwili kuanzia Julai Mosi mwaka huu, baada ya muda huo pande zote zitakutana kuangalia na kukubaliana kuongeza gharama ya pango au la kulingana na mazingira yatakavyokuwa," alisema.

Shigella pia aliagiza wafanyabiashara waliopo katika maeneo ya pembezoni mwa barabarani wapangiwe utaratibu wa kufanya biashara zao nje ya soko hilo na aliafiki maoni ya wafanyabiashara wadogo waliotaka wenzao waliopo eneo ya masoko yasiyo rasmi kuhamishiwa Soko Kuu la Chifu Kingalu ili kuzuia kutokea vurugu siku za usoni.

Mkuu huyo wa mkoa pia alipiga marufuku kutozwa ushuru wa pikipiki na bajaji zinazoingia katika soko hilo.

Mmoja wa wafanyabiashara wa mboga, Baturi Lurambo alishauri kuwekwa utaratibu bidhaa za aina moja kuwa katika eneo la wazi la chini ambazo hazitaingiliana na za ndani ili kuepuka muingiliano wa biashara na waliopo ndani kwenye vizimba.

Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga alisema maagizo yote yatafanyiwa kazi kwani itasaidia kuwa na wafanyabiashara wengi katika soko hilo tofauti na sasa.

"Pamoja na kupunguza gharama hizo, isiwe sababu ya kubweteka, tutafute mapato katika vyanzo vingine ili tufikie lengo letu la makusanyo Sh bilioni 11," alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz