Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shigela ahimiza matumizi kamba za katani

3a32814315ae73e7588d4fde7803b74a Shigela ahimiza matumizi kamba za katani

Thu, 22 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela amewataka wafanyabiashara kutii maelekezo ya serikali kwa kutumia kamba zinazotokana na katani, badala ya kuendelea kutumia za plastiki kwani zinachafua mazingira.

Alitoa kauli hiyo juzi katika ziara yake alipozuru kiwanda cha kuzalisha bidhaa za mkonge cha Tanga Sisal Spinning kilichopo eneo la Pongwe ili kujionea uzalishaji wa kamba kwa ajili ya vifungashio na matumizi mbalimbali.

Alisema serikali ilishapiga marufuku matumizi ya vifungashio ambavyo si rafiki kwa mazingira, hivyo ipo haja ya kuanza utekelezaji wa maagizo hayo kwa vitendo ili kuendelea kulinda mazingira na kutoa fursa ya viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa kwa wingi.

"Ili kukuza uchumi wa viwanda vyetu, ni vyema wafanyabiashara kuacha kutumia vifungashio vya plastiki na kuanza kujikita katika matumizi ya kamba za katani pamoja na magunia ili kuimarisha afya za walaji, lakini pia kuimarisha usalama wa bidhaa zetu," alisema.

Alisema uwekezaji uliofanywa na kiwanda wa takribani Sh bilioni tatu, unahitaji kuwekewa mazingira rafiki ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakuza soko la ndani, badala ya kutegemea kuuza nje pekee.

Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Denis Ruhinda, alisema kwa kuanzia wameajiri wafanyakazi 30, lakini wanatarajia kufikia wafanyakazi 130 kulingana na ongezeko la uzalishaji wa bidhaa.

Alisema marufuku iliyotolewa na serikali inaweza kuongeza uhitaji wa bidhaa wanazozizalisha katika soko la ndani kwani soko lao kuu ilikuwa nje ya nchi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz