Serikali Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya imeeleza sababu za magari zaidi ya 60 ya mizigo kuzuiwa nchini Malawi ni kutokana na sheria mpya za usafirishaji wa mizigo zilizopitishwa na nchi hiyo.
Akizungumza leo Jumanne, June 6, 2023 Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Josephine Manase amesema kuwa kwa sasa wanaendelea kufuatia na kutoa taarifa kwa mamlaka husika za Serikali.
“Suala hilo kwa sasa liko nje ya uwepo wetu kwani kuna sheria mpya za usafirishaji ambazo zimepitishwa katika nchi ya Malawi tunachosubiri ni Serikali ya Tanzania kukaa meza moja na Serikali ya Malawi kuweza kupata suruhisho,” amesema.
Manase amesema kwa upande wa uongozi wa wilayani ni kuendelea kufuatilia nini kinaendelea na kuwasilisha katika mamlaka husika za Serikali lakini wanatarajia suala hilo litashughulikiwa na magari yaliyozuiwa kuruhususiwa kuingia nchini kupitia kituo cha pamoja cha forodha.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema bado Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na nchi jirani ya Malawi ili kupata suruhisho na shehena za mizigo ziweze kiruhusiwa kuingia nchini.
Diwani Kata ya Njisi mpakani mwa Tanzania na Malawi, Omary Rashid ameomba Serikali kufanya kila linalowezekana kuondoa mkwamo huo kwani utaleta athari kubwa kiuchumi kwa wafanyabishara waliokuwa wakisafirisha bidhaa kuleta nchini.
Juni 5, 2023 wafanyabishara wa eneo la Kasumuru Mpaka wa Tanzania na nchi jirani ya Malawi walipanga magogo barabarani kushinikiza magari zaidi ya 60 yaliobeba shehena za mizigo yaliyozuiwa nchini humo kuachiwa.
Hatua hiyo imekuja baada ya magari hayo kuzuiwa zaidi ya mwezi na nusu na kupelekea mazao yanayosafirishwa kuwa katika hatari kubwa ya kuharibika.