Wakazi wa Kata ya Shambarai wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamewalalamikia viongozi wa Kata ya Shambarai Burka wilayani Arumeru mkoani Arusha, kwa kuanzisha mnada na soko jirani na mpaka wao hadi kuwasababishia mnada wao kufa.
Baadhi ya wakazi hao wameiomba Serikali kuingilia kati suala hilo ili kulirejesha kwao soko na mnada huo kwani wenyewe waliuanzisha tangu miaka ya 1970 ila Shambarai Burka wakaanzisha miaka ya 1990. Mkazi wa kijiji hicho Eliaman Stephano, akizungumza Juni 26 amesema wananchi wa kata ya Shambarai wana nyaraka za uanzishwaji soko na mnada wao ila majirani zao hawana vibali.
"Mnada wetu ulikuwepo tangu enzi Rais wa Tanzania akiwa Julius Nyerere haiwezekani watu wengine waanzishe mnada wao jirani na sisi na kuua soko na mnada wetu wa miaka mingi Serikali iingilie kati jambao hili," amesema. Mkazi wa kijiji hicho Japhet Daniel amesema baadhi ya wananchi wa eneo hilo walichukua mikopo maeneo tofauti kwenye taasisi za fedha ila wanashindwa kurejesha baada ya mnada huo kufa.
"Watu wamechukua mkopo kufanya biashara, hii ni hujuma inafanyika kwani huwezi kuondoka hapa uende jirani na Kijiji cha Naberera ukaanzisha soko pale hivyo hatua zichukuliwe ili kunusuru soko hili la Shambarai," amesema Daniel. Mwenyekiti wa Kijiji cha Shambarai Merinyo Mollel amesema wizara husika iingilie changamoto hiyo kwani sheria za minada na masoko inaagiza kuanzisha mnada mwingine umbali wa kilomita saba na uliopo ni kilomita nne. Mwenyekiti mstaafu wa kijiji hicho Edward Kinyonga ameiomba serikali kuingilia kati suala hilo kwani miundombinu iliyopo inaharibika kwa kutotumika na kukosa usimamizi. Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Shambarai Burka wilayani Arumeru mkoani Arusha, John Mollel amewataka wakazi wa kata ya Shambarai ya wilayani Simanjiro mkoani Manyara, kuboresha soko na mnada wao ili wateja waamue wenyewe sehemu ya kwenda.