Serikali imekamilisha mradi mkubwa wa maji wa Rundugai ambao umegharimu Sh97.6 milioni wilayani hapa ambao unahudumia zaidi ya wananchi 9,500 kutoka Vijiji vya Kawaya, Rundugai, Cheki Maji, Kilimambogo na sehemu ya Kijiji cha Chemka.
Hayo yamebainishwa wakati Mwenge wa uhuru ulipofika kuzindua tanki la maji la lita 100,000.
Akisoma taarifa ya utekekezaji wa mradi huo, Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Emmanuel Mwampashi amesema mradi huo umetekelezwa kwa fedha za Serikali kupitia Mfuko wa Maji wa Taifa.
Kwa mujibu wa meneja huyo, makadirio ya mradi yalikuwa ni Sh111.1 milioni japo wamepokea Sh100 milioni, huku zikitumika Sh97.6 milioni ambazo zimekamilisha mradi na wananchi wameanza kupata huduma hiyo bila tatizo.
Akizindua mradi huo, Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa, Abdalla Shaib Kaim amesema baada ya kupokea taarifa na kukagua mradi pamoja na kuangalia thamani ya fedha, wameridhika mradi uko vizuri na umezingatia viwango vya ubora.
"Tumefanya ukaguzi wa kina wa mradi na nyaraka lengo likiwa ni kuona kama mradi umezingatia viwango vya ubora na kama thamani ya fedha inaakisi na kuendana na mradi husika, tunafanya hivyo kwa dhamira njema ili kuona fedha ya watanzania inakwenda kuleta tija katika miradi ya maendeleo na kutimiza dhamira ya serikali ya kumtua mama ndoo kichwani"
Kwa upande wa Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe amesema kukamilika kwa mradi huo ni mkombozi mkubwa kwa wananchi kwa kuwa wanakwenda kuondokana na adha ya kuzunguka usiku na mchana kutafuta huduma ya maji.
"Eneo hili palikuwa na shida kubwa ya maji na wananchi waliteseka kusaka huduma hii, lakini serikali imetoa fedha ambayo imetekeleza mradi huu mkubwa ambao umewatua kina mama ndoo kichwani," amesema.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanawake wamesema awali walitoka asubuhi kwenda kutafuta maji na kurudi usiku, hali ambayo ilisababisha migogoro na waume zao na kuhararisha ndoa zao lakini kukamikika kwa mradi huo, kutaimarisha familia.
"Mradi huu wa maji kukamilika ni mkombozi mkubwa kwetu wananchi hasa kina mama, kwani tulitembea zaidi ya kilometa tano kutafuta maji, wakati mwingine tulitoka asubuhi na kurudi jioni au usiku, jambo ambalo lilihatarisha ndoa zetu na hata maisha," amesema Mwanaisha Salim na kuongeza;
"Ukosefu wa maji ulikwamisha pia watoto kwenda shule kwa sababu ya kupeana zamu za kwenda kuhemea maji, hili lilikuwa tatizo ambalo lilitukwamisha kimaendekeo, lakini kwa sasa tumepata huduma ni jambo ka kushukuru."
Naye Juma Bakari amesema walitumia gharama kubwa na muda mwingi kusaka huduma ya maji, lakini sasa wameweza kufikishiwa huduma karibu, hali ambayo inawapa fursa ya kufanya shughuli nyingine za maendeleo na kujikwamua kiuchumi.
"Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea huduma hii ya maji kwa kuwa hapo awali tulitumia gharama kubwa na muda mwingi kutafuta maji hivyo hata muda wa kutafuta maendeleo ulikua mdogo," amesema.