Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sh9 bilioni kuboresha upatikanaji maji Mtwara

Maji Sh9 bilioni kuboresha upatikanaji maji Mtwara

Wed, 25 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Miradi saba ya maji yenye thamani ya Sh9 bilioni, itakayowanufaisha zaidi ya wakazi 65,000 katika vijiji 35 mkoani Mtwara, iko mbioni kutekelezwa na hivyo kutimiza lengo la kitaifa la kusambaza huduma za maji vijijini kwa asilimia 85.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) mka huo, Primy Damas, amesema kwa sasa wakala huo umefanikiwa kusambaza maji vijijini kwa asilimia 67.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa miradi hiyo, meneja huyo amesema kuwa miradi hiyo inaenda kuongeza kiwango cha upatikanaji maji katika Mkoa wa Mtwara.

Ameitaja miradi kuwa ni ule wa Maundo ambao utanufaisha wananchi zaidi ya 39,000 kutoka katika vijiji 16 wenye thamani ya Sh5.9 bilioni, pia upo mradi wa Chitohori utakaogharimu Sh1.4 bilioni, ambao utanufaisha watu 10,947.

Mradi mwingine ni ule wa Makome, Mnyundo, Mwatei wa vijiji vinne watu zaidi ya 3000 wenye thamani ya Sh1 bilioni.

Aidha ameongeza kuwa upo mradi wa Mahurunga wenye thamani ya Sh800 milioni, ambao utanufaisha zaidi ya watu 5000, pamoja na mradi wa Dihimba utakaowanufaisha watu 4000 wenye thamanai ya Sh600 milioni.

Kwa mujibu wa Meneja huyo, mradi mwingine ni wa Kijiji cha Ngonja Navikole wa thamani ya zaidi ya Sh4 milioni pamoja na mradi wa Mayembe - Mchanje wenye thamani ya Sh4 milioni.

“Mbali na miradi hiyo pia ipo mikubwa mitatu ya kimkakati ambayo ni Makonde Newala Tandahimba na Nanyamba, iliyofikia asilimia 20 ya utekelezaji, huku ule wa kutoa maji Mto Ruvuma kwenda katika Mji wa Mangaka, wenye thamani ya Sh38 bilioni, upo katika hatua ya utekelezaji,” amesema na kuongeza;

“Kwa hapa mjini tunao mradi wa uboreshaji wa miundombinu na usambazaji wa maji mjini wenye thamani ya Sh18 bilioni upo kwenye utelekezaji pamoja na mradi wa Mnyawi wenye thamani ya Sh5 bilioni.”

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas amesema kuwa miradi hiyo inapaswa kusimamiwa kwa weredi na kukamilika kwa wakati ili iweze kuwasadia wananchi.

“Ni muhimu viongozi hakikisheni miradi inakamilika kwa ubora na kwa thamani iliyokusudiwa, tunaamini kuwa kukamilika kwa mirdi hii kunaenda kuwatua ndoo kichwni wakina mama. Kwa wakandarasi, kazi ndio imeanza kamilisheni kwa wakati bila kuharibu viwango vya utekelezaji wa miradi hiyo” amesema Kanal Abbas

Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Patrick Sawala amesema kuwa upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo ulikuwa ni asilimia 28 ambapo ndani ya miaka miwili imepanda hadi kufikia asilimia 53.

“Upatikanaji wa maji ulikuwa chini ya asilimia 28 miaka kadhaa nyuma, maji yalikuwa ni changamoto kubwa na katika kipindi cha miaka miwili, hata hivyo, hali ya upatikanaji maji kwa sasa imeboreshwa hadi kufikia asilimia 53,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mwanahamisi Munkunda amesema: “Tunafarijika kuona zaidi ya Sh9 bilion zikitolewa kwa ajili ya miradi ya maji, na sisi tumepata ujenzi wa matenki, na uboreshaji wa miundombinu, ni shauku yetu kuona kila mtu awe na uhakika wa maji nyumbani kwake.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live