Serikali imetenga zaidi ya Sh390 milioni kukabiliana na uhaba wa maji katika mji wa Holili, wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro, baada ya kuanza kutekeleza mradi wa maji Mawanda, ambao utakamilika Julai mwaka huu.
Mradi huo utakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi 12,900 ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakipata mgao wa maji kwa wiki mara moja.
Akizungumzia mradi huo jana Februari 22, Mbunge wa Rombo, ambaye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema mradi huo utakapokamilika utapunguza changamoto ya maji kwa kiasi kikubwa katika Mji wa Holili huku wakiendelea kutafuta vyanzo vingine vya maji.
"Holili ni mji ambao unakuwa kwa kasi kubwa sana, na idadi ya watu inaendelea kuongezeka, mradi huu wa maji ambao uko hapa utakapokamilika angalau utapunguza changamoto ya maji japo uhitaji wa maji katika mji huu ni mkubwa sana," amesema.
Amesema licha ya mradi huo kukamilika, bado uhitaji wa maji ni kubwa hivyo wanaangalia namna ya kutafuta vyanzo vingine vya maji ili wananchi wa eneo hilo waweze kupata maji yakuwatosheleza.
"Nimeongea na Waziri wa maji, Jumaa Aweso na nimemwomba tutafute vyanzo vingine vya maji kutoka katika maeneo mengine ili tuweze kupata maji mengi, maana mgao wa maji katika hili eneo ni mkubwa mno.
"Tunamshukuru sana Rais wetu, Samia Suluhu Hassan kwa kuweka kipaumbele kwenye suala la maji, na mimi nitahakikisha miradi ya maji hapa Rombo haichezewi, hatutakuwa na utani na mtu yeyote katika hili,
“Leo nimeongea na bodi ya maji ya Rombowasa nikawaambia tutawatetea watumishi na kuwalinda lakini sisi tunataka tuone matokeo, Warombo wanachotaka ni maji," amesema.
Festo Joseph, kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Rombo (Rombowasa), amesema mahitaji ya maji katika mji wa Holili ni lita za ujazo 3,200 kwa siku huku mradi huo wa maji ukizalisha lita za ujazo 691 sawa na upungufu wa lita 1,800. "Mradi huu wa maji utakamilika Julai mwaka huu na utakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi 12,900 hapa mji wa Holili, lakini mahitaji ya maji hapa ni makubwa.
“Huu mradi utazalisha lita za ujazo 691 kati ya lita 3,200 kwa siku hivyo tuna upungufu wa lita 1,800, tutachimba visima viwili vya maji kule Holili ambapo itaondoa kabisa kero ya maji," amesema.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Rombo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Gilbert Tarimo, amemshukuru Mbunge wa Rombo, Profesa Mkenda kwa jitihada kubwa anazozifanya kwenye miradi ya maji ambayo itatatua changamoto kubwa ya maji katika wilaya hiyo.
"Rombo imekuwa na changamoto kubwa ya maji, tunaishukuru serikali yetu kwa kupitia mbunge wetu wa Rombo tumepata Sh10 bilioni kwa ajili ya miradi ya maji, sisi kama halmashauri tutahakikisha fedha hizi zinatumika vizuri ili maji yaweze kupatikana kwa wananchi,” amesema.