Dar es Salaam. Zaidi ya Sh340 bilioni imetumika kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya shule za msingi na sekondari nchini Tanzania katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Olenasha leo Alhamisi Februari 27, 2020 wakati akizindua usambazaji wa vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza kwa ajili ya shule za mchepuo huo.
Vitabu vingine vilivyoanza kusambazwa ni vilivyoandikwa kwa mfumo wa nukta nundu na vilivyokuzwa maandishi kwa ajili ya wanafunzi wasioona na walio na uoni hafifu.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Olenasha amesema usambazaji wa vitabu shuleni ni kati ya mkakati ya kuboresha elimu inayoenda sambamba na kazi za ukarabati na ujenzi wa shule.
"Maudhui ya elimu yapo ndani ya vitabu hivyo hatuishii kujenga na kukarabati shule tu isipokuwa pamoja na kuhakikisha maudhui yanakuwepo shuleni," amesema.
Amewataka wamiliki wa shule binafsi kutumia vitabu hivyo katika kufundishia ili waende sambamba na mtalaa wa elimu.
Pia Soma
- Henga: Watumishi LHRC tunatishiwa
- Jinsi wahitimu mafunzo benki walivyowasaidia viziwi
- Ndege za abiria kutoka China kutua Kenya
Amesema vitabu vilivyosambazwa ni vya wanafunzi wa darasa kwanza mpaka la sita kwa mchepuo wa Kiingereza na shule ya msingi mpaka sekondari kwa wanafunzi wasioona.
Amezitaka shule zote nchini kutumia vitabu vyenye ithibati kwa ajili ya kufundishia na si vinginevyo.