Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sh11 bilioni zachangwa kuboresha miradi ya elimu

Sun, 25 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Zaidi ya Sh11 bilioni zimechangwa na wadau, taasisi mbalimbali za serikali na za binafsi katika kuchangia miradi mbalimbali ya elimu nchini katika kipindi cha 2015 na 2018.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Novemba 23,2018 wakati wa kukabidhi hati za utambuzi wa elimu kwa wachangiaji miradi ya elimu ambapo jumla ya taasisi 18 zimetunukiwa.

Akizungumza wakati wa kukabidhi hati hizo, Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema fedha hizo zimetumika katika kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa madarasa, maktaba, ununuzi wa vifaa vya ICT, madawati na ukarabati wa shule.

"Yapo mengi yaliyofanyika kupitia fedha hizo ambayo yamesaidia kuboresha elimu kwa watoto wetu katika ngazi mbalimbali na kuwafanya baadhi yao kusoma katika mazingira ya kuvutia zaidi," amesema Ole Nasha..

Amesema kutokana na mwamko huo ni mategemeo yake kuwa mwaka 2019 idadi ya taasisi zitakazojitokeza katika kuchangia miradi ya elimu itaongezeka zaidi.

"Wakati wadau wakijitahidi kutusaidia kuboresha miradi mbalimbali na sisi kama wizara tunafanya kila tunaloliweza ili kuhakikisha tunaendana na kasi ya udahili wa wanafunzi," amesema Ole Nasha.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (Tea) Profesa Maurice Mbago amesema mbali na kuwepo kwa baadhi ya watu waliochangia miradi mbalimbali ya elimu ila bado mwamko wa wadau ni mdogo.

"Ila tunaamini kadri siku zinavyokwenda na uhamasishaji unaofanyika tutaweza kupata fedha nyingi zitakazosaidia kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu," amesema Profesa Mbago.



Chanzo: mwananchi.co.tz