Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa amesema kuwa Rais Samia Suluhu amekubali ombi la wananchi wa kijiji cha Laja la kujengewa daraja ambalo litawaunganisha na tarafa ya Eyasi ili kuondoa adha ya kukwama kuvuka korongo la kuunganisha maeneo hayo nyakati za mvua.
Waziri Mchengerwa amesema hayo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Bora na Serikali ya Mitaa ilipotembelea kijiji cha Laja kuzindua daraja lililojengwa na TASAF na wananchi kuomba kujengewa daraja jingine ili kuondoa ya kukwama kufika eneo ya Eyasi.
Mchengerwa amesema Rais Samia Suluhu anataka kuona wilaya ya Karatu inabadilika na kupata maendeleo ya kasi, ndio sababu ameahidi pia kuwajengea daraja jingine.
"Kutokana na maombi yenu hapa, nimeongea na Rais Samia Suluhu amekubali atajenga daraja kuunganisha Laja na Eyasi kama ambavyo mmeomba na naagiza TASAF kuanza kufanya tathimini kushughulikia suala hili "amesema
Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Abdalah Chaurembo aliwataka viongozi wa Karatu kuanza mara moja kazi ya ufatiliaji na baadaye ujenzi wa kivuko ambacho Rais ameahidi wananchi.
"Ndani ya mwezi mmoja kamati itataka kujua mmefikia wapi, tunataka Karatu sasa ikimbie baada ya kuwa nyuma katika maendeleo na tutafatilia kwa karibu miradi yote ya TASAF hapa ili kuhakikisha wananchi wananufaika na tukibaini tatizo tutachukuwa hatua"amesema.
Mbunge wa Karatu, Daniel Awakie alisema wilaya ya Karatu inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwepo tatizo la uhaba wa miundombinu na hivyo akaomba Serikali kusaidia kutatua kero hiyo.
“Tunashukuru leo kuzinduliwa daraja hili lakini pia Rais kukubali maombi yetu na kujenga daraja lingine kuunganisha Laja na tarafa ya Eyasi jambo hili litainua uchumi wa Karatu"amesema.