Kwimba. Serikali imetenga Sh1.5 bilioni kujenga Chuo cha Elimu ya Ufundi (Veta) Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Tanzania ili kuwasaidia vijana wapate ujuzi wa mambo mbalimbali, hatua itakayosaidia kukabiliana na ukosefu wa ajira na kuzurura mitaani.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Julai 6, 2019 na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha alipotembelea na kukagua shughuli za uboreshaji wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Malya, wilayani hapa.
Amesema lengo la Serikali ni kujenga vyuo vya ufundi katika wilaya 25 nchini, lengo likiwa ni kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana.
“Fedha hizi tayari zimeshatengwa kwa ajili ya shughuli hiyo na lengo la Serikali ni kujenga vyuo hivyo katika wilaya 25 nchini, hii ni kwa ajili ya kuwajengea uwezo vijana wakapate ujuzi ambao utaweza kuwasaidia kwenye maisha na kuongeza pato,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Pendo Malebeja amesema tayari eneo limeshatengwa lakini wanakamilisha taratibu za umiliki wa hati kutoka kwenye halmashauri na kuwa kwenye miliki ya Veta.
Amesema, “Tumeshamaliza taratibu zote kilichobaki ni kujaza fomu za mikataba ambazo wakati wowote tunaweza kujaza. Naibu Waziri amewataka wafanye haraka kumaliza taratibu hizo ili ujenzi uanze mara moja.
Pia Soma
- Viongozi wawili Chadema wadaiwa watekwa
- Makubaliano ya Rais Magufuli, Kenyatta haya hapa
- Lugola awashukia polisi wanaowadhulumu wananchi ardhi
Mkuu wa chuo cha Maendeleo Malya, Frank Josephat amesema wamepokea Sh445 milioni kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya chuo hicho, ambacho kwa mwaka huu wamedahili wanafunzi 138 lakini wanakabiliwa na changamoto ya vitendea kazi, bweni na uhaba wa wakufunzi kwa ajili ya kutoa elimu inayostahili.