Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sh bilioni 9.1 zalipwa ujenzi Makao Makuu ya Uhamiaji Dodoma

218c52d5d308d90014bda5c9bb0d55b8 Sh bilioni 9.1 zalipwa ujenzi Makao Makuu ya Uhamiaji Dodoma

Sat, 26 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JUMLA ya Sh bilioni 9.1 zimelipwa na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) ikiwa ni sehemu ya malipo ya gharama ya ujenzi wa makao makuu ya Uhamiaji jijini Dodoma.

Mhandisi wa mradi huo wa ujenzi utakaogharimu Sh bilioni 20, Issa Mohammed ametoa taarifa hiyo kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo wakati wa ziara ya ukaguzi.

Mradi unatarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu.

“Lengo letu ni kumaliza mradi huu katikati ya Oktoba, pamoja na kuzingatia muda, bado tunachukua tahadhari kubwa kuhakikisha ubora na uimara unaotegemewa kufikiwa kuanzia kwenye msingi hadi kukamilisha mradi mzima,” alisema.

Kwa mujibu wa Mohammed, wameshalipwa Sh bilioni 9.1 ikijumuisha malipo ya awali kwa ajili ya watoa huduma ambayo thamani yake ni Sh bilioni 1.3.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Chilo alisema miradi iliyoachwa na Rais John Magufuli ni muhimu imalizwe na fedha hizo ambazo ni za Watanzania, zitumike ipasavyo.

“Miradi hii imetumia fedha nyingi tena fedha zetu za ndani,ifike wakati miradi hii ikamilike maana hakuna fedha iliyotoka nje kwa maana msaada kwa hiyo kazi iendelee ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema.

Aliwaomba wafanyakazi kufanya kazi usiku na mchana jengo hilo lianze kutumika kama lilivyokusudiwa, Mradi huo ulianza rasmi Mei 28, mwaka 2019, unajumuisha ujenzi wa jengo la ofisi yenye urefu wa ghorofa nane na sakafu ya chini, uwekaji wa mifumo ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na kusawazisha ardhi ya nje ya jengo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz