Serikali imetoa kiasi cha Sh milioni 800 kwa ajili ya kujenga shule mpya ya msingi katika mtaa wa Mwatulole, Kata ya Buhalahala ambayo itakuwa shule ya mfano katika Halmashauri ya mji wa Geita.
Akisoma taarifa ya mradi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Geita , Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwatulole, Catherine Mugusi amesema mradi huo unalenga kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Amefafanua, kati ya fedha hizo, kiasi cha Sh milioni 690.7 ni fedha ya ununuzi wa vifaa, huku sh miloni 109.3 ni gharama za ufundi, ambapo hadi sasa sh milioni 477.3 imeshatumika kwa malipo ya mradi.
MKUU wa mkoa wa Geita, Martin Shigella (katikati) akizungumza baada ya kukagua mradi wa shule ya mfano katika kata ya Buhalahala mjini Geita.(Picha zote na Yohana Shida).
Ameeleza, hadi sasa mradi umekamilika kwa asilimia 60, na majengo yote yapo kwenye hatua ya upauaji, na ikikamilika utaondoa msongamano kwenye shule mama za Mwatulole na nguzo mbili.
Ofisa Elimu Maalum Msingi, Halmashauri ya Mji wa Geita, Zunaeda Alphonce amesema, mradi una vyumba vya madarasa 20, maktaba, matundu ya vyoo 20 na jengo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Amesema shule hiyo itaondoa msongamano kwani shule za Msingi Nguzombili na Mwatulole zina takribani wanafunzi 10,000, ambapo pia kupitia mradi wa BOOST shule hizo mbili zimepatiwa Sh milioni 500.
Aliongeza, halmashauri pia wamepokea Sh milioni 55 kutoka serikali kuu kupitia mradi wa LANES na zimepelekwa kwenye mradi wa shule ya mfano, ili kujenga vyumba vya mfano kwa madarasa ya awali.
Diwani wa Kata ya Buhalahala, Dotto Zanzui amekiri, mradi wa shule ya mfano utaongeza hamasa kwa wanafunzi kujifunza kwenye mazingira rafiki na kuinua kiwango cha taaluma ndani ya kata hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amesema huo ni mwendelezo wa sera ya serikali ya awamu ya sita kuboresha sekta ya elimu na kuwataka wasimamizi wa miradi huo uweze kukamilika kwa utimilifu.