Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali katika kutatua changamoto za mawasiliano nchini ambapo katika Wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe inatarajia kutumia shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano.
Amesema hayo jana (Novemba 27, 2022) katika Kijiji cha Mawengi kilichopo wilayani humo wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua miundombinu ya miradi ya mawasiliano, usikivu wa TBC na miradi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).
“Serikali imetenga fedha shilingi bilioni 1.8 zitakazotumika kwa ajili ya kujenga minara katika kata sita za Iwela, Ludende, Monde, Milo, Mawengi na Lujelawa, huu ni uwekezaji mkubwa utakaofanywa na Serikali ambao utatatua changamoto za mawasiliano katika wilaya hii”. Amesema Mhe. Naibu Waziri Kundo.
Ameongeza kuwa tayari kata hizo sita zimeingizwa katika mfumo wa kutafuta mzabuni kwa ajili ya ujenzi wa minara ili kutatua changamoto ya mawasiliano katika Jimbo la Ludewa. Ambapo katika Kata ya Ibumi ulipo mnara wa TTCL jitihada zinafanyika ili pia mnara huo uweze kutoa huduma.
Akifafanua faida za uwepo wa minara hiyo ya mawasiliano, Mhe. Naibu Waziri huyo amesema “Baada ya miradi hiyo kukamilika mtapata huduma za kupiga simu, kutuma ujumbe mfupi pamoja na intaneti hivyo mtaweza kujifunza masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya biashara na muhimu zaidi ni kuwa mawasiliano haya ni muhimu hasa katika maeneo haya ya mpakani.”
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Mhe. Joseph Kamonga ameishukuru Serikali kwa kuendelea kufanya jitihada mbalimbali za kutatua changamoto ya mawasiliano katika Jimbo la Ludewa.
“Tumeweza kupata mnara kutoka katika Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za Mkononi ya Airtel katika maeneo ya Ilawa na Mkongebaki, vilevile mnara wa Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za Mkononi ya Tigo katika maeneo ya Mkomeng’onde na Ngalawale kwa kipindi hiki kifupi tumepata minara nane, naishukuru sana Serikali hivyo tunaamini baada ya ujenzi wa minara mingine iliyosalia huduma za mawasiliano zitapatikana vizuri zaidi hapa Ludewa na kufungua fursa mbalimbali,” ameeleza Mhe. Kamonga.
Mkazi wa Ludewa, John Edmund ameeleza kuwa wananchi wa eneo hilo wamefurahishwa na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali za kuboresha huduma ya mawasiliano wilayani humo.
“Hakuna aliyetegemea eneo hili la pembezoni kama litakuwa na mawasiliano, hii ni kama ndoto tunaishukuru Serikali kwani tutaweza kuwasiliana vizuri zaidi pamoja na kufahamu taarifa za masuala mbalimbali yanayoendelea ya kitaifa na kimataifa," ameeleza Bw. Edmund.