Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yazuia udhalilishaji ukaguzi Mirerani

335e53aa59504d7651440e151a8c9654.jpeg Serikali yazuia udhalilishaji ukaguzi Mirerani

Wed, 17 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imepiga marufuku upekuzi unaodhalilisha kwa wachimbaji na wafanyabiashara wanaopita katika lango kuu la ukuta uliozunguka mgodi wa madini ya tanzanite katika mji wa Mirerani wilayani Simanjiro katika Mkoa wa Manyara.

Waziri wa Madini, Dotto Biteko alitoa marufuku hiyo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na kuzitaka mamlaka zinazohusika na ukaguzi huo kuangalie namna bora ya kulinda heshima na utu wa binadamu.

Biteko aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, serikali inaboresha upekuzi katika lango hilo ikiwa ni pamoja na kufunga mitambo ya kisasa ili kuondoa malalamiko.

Alionya dhidi ya tabia ya baadhi ya wachimbaji kutorosha madini na kusema kuanzia sasa, watakaokamatwa watapigwa picha na picha hizo zitabandikwa katika ubao wa matangazo na kisha watapigwa marufuku kukanyaga eneo hilo kwa mwaka mmoja.

Biteko alisema serikali itaweka utaratibu wa kukagua wachimbaji katika lango kuu ili wakagiliwe haraka na bila kudhalilishwa.

Alisema serikali inakamilisha jengo la kisasa la ukaguzi litakalofungwa mitambo ili litumike kwa ukaguzi wa faragha kwa wachimbaji wanaokwenda nje ya lango hilo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula, alisema kamati hiyo imeridhishwa na namna serikali inavyodhibiti utoroshwaji madini katika mgodi huo.

Alisema, ujenzi wa mifumo ya ulinzi ukiwemo ufungaji wa kamera za CCTV na ujenzi wa barabara ya ndani inayozunguka ukuta, umedhihirisha mapendekezo yanatekelezwa vizuri.

"Baada ya kutembelea mgodi huu, tumeridhika na udhibiti wa utoroshwaji wa madini, lakini tunapendekeza adhabu kali zitolewe kwa watu wanaoendelea na tabia ya kutorosha madini," alisema.

Kitandula alisema kamati imeridhishwa na namna ukuta ulivyosaidia kuimarisha ulinzi na kuzuia utoroshwaji wa madini ya tanzanite, hivyo kukuza mapato ya serikali.

"Sisi kamati tumejionea mambo mbalimbali yanayoendelea hapa, kimsingi serikali inataka mapato kupitia kamati yetu, tutajitahidi kuiambia serikali iweke mitambo ya kisasa eneo la lango kuu," alisema.

Mjumbe wa kamati hiyo, Christopher Ole Sendeka ambaye ni Mbunge wa Simanjiro, alikemea tabia ya baadhi ya wachimbaji wadogo kutorosha madini na akatoa mwito kwa serikali kufungua migodi mikubwa na midogo ili kukuza ajira na kukuza mapato ya nchi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz