Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatoa tani 300 za mahindi kuwanusuru wananchi Monduli

Maguni Ya Mahindi Serikali yatoa tani 300 za mahindi kuwanusuru wananchi Monduli

Tue, 25 Oct 2022 Chanzo: Mwananchi

Serikali imetoa jumla ya tani 300 za mahindi kwa ajili ya kugaiwa wananchi wilayani hapa waliokumbwa na ukame uliosababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Wananchi wa wilaya ya Monduli kwa sasa wanapitia hali ngumu ya maisha kutokana na sehemu kubwa ya ardhi yao kukumbwa na ukame uliokausha vyanzo vingi vya maji na malisho kwa misimu mitatu mfululizo.

Akizungumza jana Oktoba 24, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe amesema wananchi wa wilaya yake wanapitia hali ngumu kutokana na ukame uliosababishwa na mvua kutonyesha misimu mitatu na kupelekea kuwa na uhaba wa chakula.

"Kamati ya Usalama na Maafa wilaya tulikaa na kuona tatizo lipo ndio tukaongea na Waziri wa kilimo (Hussein Bashe) ambaye baada ya kumpelekea mahitaji yetu ya tani 3,000 kunusuru wananchi ambao hawana uwezo wa kununua chakula kutokana na bei kuwa juu, akatupatia mahindi hayo," amesema.

Mwaisumbe amesema chakula hicho kitauzwa kwabei rafiki ya Sh800 kwa kilo badala ya 1,200 hadi 1,500 wanayouziwa sokoni.

"Kama hizo tani zitaonekana hazitoshi tutaendelea kutoa taarifa kupata mahindi zaidi ndani ya hizo tani 3,000 tuliyoomba ili tuone uwezo wa wananchi katika kununua kuliko kuleta yote na kuja kurundika”…

Amesema kuwa mahindi hayo watagawa katika vijiji 62 vilivyoko kwenye vitongoji 300 vya wilaya nzima kwa utaratibu wa viongozi wa ngazi za chini ili kuepuka wenye nia ovu ya kununua mengi na kwenda kuyafanyia biashara kwa manufaa yao binafsi.

Mmoja wa wananchi wa wilaya ya Monduli, Lalashe Leisoi amesema kuwa kupata chakula hicho kitaweza kuwanusuru familia zao ambazo ziko katika hali mbaya kiafya kutokana na kushindia mlo mmoja kwa siku.

"Baadhi ya mifugo yetu imekufa kwa kukosa malisho huku sisi wenyewe hali ikiwa mbaya sana ambapo katika kujinusuru tumekuwa tukibadilishana mbuzi na wao kutupa debe mbili za mahindi ambayo yamekuwa yakitusogeza," amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuishukuru serikali kwa msaada wa mahindi huku wakiomba wadau wengine kujitokeza kusapoti juhudi hizo Ili waweze kupata maji na chakula.

Chanzo: Mwananchi