Mbozi: Serikali mkoa wa Songwe imetoa majeneza 19 kwa ajili ya kuhifadhia miili ya watu 19 waliofariki kwa ajali usiku wa kuamkia leo Ijumaa Februari 22, 2019 katika Mlima Senjele wilayani Mbozi mkoani hapa.
Akizungumza leo, mkuu wa wilaya ya Mbozi, John Palingo amewaambia waombolezaji waliofika katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Serikali ya mkoa wa Songwe (Vwawa) kuwa kazi ya kutambua miili hiyo inasimamishwa kwa muda ili kupisha wataalamu waiweke vizuri miili hiyo iliyoharibika vibaya.
“Serikali ya mkoa imetoa majeneza hayo ili kuweza kuistiri vizuri miili kisha baada ya hapo kazi ya kuitambua itaendelea kama kawaida,” amesema Palingo.
Mmoja wa ndugu wa marehemu hao, Robert Mwakilemile ameutambua mwili wa baba yake aitwaye Sunday Mwakilemile mkazi wa Mwanjelwa Mbeya ambaye enzi za uhai wake alikuwa akifanya kazi ya udereva katika mji wa Tunduma lakini jana alikuwa katika safari ya kawaida akiitembelea familia yake mjini Mbeya.
Soma zaidi: Ajali ya lori, Coaster yaua abiria wote 19
Amesema kwa mara ya mwisho aliwasiliana na mama yake saa mbili usiku akamwambia wanaendelea na safari na kwamba muda huo walikuwa katika mji wa Mlowo.
Naye Hassan Mwashambwa amesema ameutambua mwili wa shemeji yake mume wa mdogo wake aitwaye Joseph Mbwama mkazi wa Mbeya ambaye alikuwa ametokea Mlowo kwenda Mbeya.
Amesema marehemu alikuwa fundi mwashi katika mji wa Mlowo ambako amekuwa akisafiri kila siku asubuhi na kurudi jioni nyumbani kwake.
Mmoja wa watu waliofika kutambua miili ya marehemu hao, Jenifa Daudi amesema hili ni tukio baya kubwa kutokea na kwamba limewastua wengi na kusababisha taharuki katika mji wa Vwawa na maeneo jirani ya Tunduma, Mlowo na Mbeya.
Soma Zaidi: Wananchi wafurika kutambua miili ya ndugu zao ajali Songwe