Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yashauriwa kuhusu miundombinu makazi ya milimani

Slum Tourism Mwanza 1 Serikali yashauriwa kuhusu miundombinu makazi ya milimani

Tue, 24 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imeshauriwa kuboresha miundombinu rafiki ikiwemo barabara kuwezesha makazi ya maeneo ya milimani jijini Mwanza kufikika kirahisi.

Ushauri huo umetolewa jijini Mwanza na Meneja Kanda ya Ziwa kampuni ya Bima Jubilee Allianz, Amina Elmy wakati wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo mawakala wa bima akisema kufikika kwa makazi hayo kutawawezesha wananchi kukatia bima nyumba zao.

Amesema makazi ya maeneo ya mlimani yana nyumba nzuri na zenye thamani zinazostahili kukatiwa bima, lakini makampuni mengi ya bima yanaogopa kuchangamkia fursa hiyo kutokana na changamoto ya miundombinu, hasa wakati wa dharura ya majanga ya moto.

Amina amesema kwa sasa kampuni za bima zimekuwa zikiogopa kufanya biashara hiyo na wateja wenye nyumba na majengo mengine maeneo ya milimani kwa hofu ya kuingia hasara kubwa majanga yanapotokea kwani maeneo hayo hayana miundombinu rafiki itakayosaidia vyombo vya uokoaji kufika na kutoa msaada kwa wakati.

“Kampuni zina hofu ya kupata hasara kuwa na wateja hao hivyo nashauri Serikali iboreshe miundombinu hasa barabara zinazoweza kufikika huko ili irahisishe kupatikana msaada wakati wa majanga na hii itasaidia kila mtu alipo aweze kunufaika na bima,” amesema Amina

Wawakala Perison Mlote, mkazi wa Mwanza, amesema; “tunaomba mamlaka zitusaidie kwa sababu huko milimani watu wana majengo mazuri na yanapaswa kuwa na bima lakini ni ngumu kufanya biashara hiyo kutokana na uwezekano mkubwa wa hasara (Risk Exposure), kwahiyo miundombinu mizuri na rafiki itatusaidia wapate bima za makazi yao,”

Meneja Mkuu wa Mawakala kampuni ya Jubilee Allianz, Mary Ndege, alisema ni muhimu kwa wananchi kuwa na bima kwani inaondoa umaskini kwa kumrudisha mteja katika hali yake ya mwanzo baada ya kupata janga, na inasaidia kuleta amani kiuchumi, kijamii na kisaikolojia.

“Tunahitaji wakala wa Jubilee awe wa tofauti anapodili na mteja basi atamani kuja kwako na siyo kwingine kwahiyo hakikisha unawapa taarifa zote muhimu kwa sababu tuko kwenye biashara ya kuwahudumia watu huku tukiwapa bima ni lazima uwajali kwanza ili kuwapa huduma nzuri na uuze bidhaa yako,” alisema Meneja huyo

Mmoja wa mawakala waliofanya vizuri na kuzawadiwa runinga mbili na printa, Justin Njelwa, mkazi wa Mwanza amesema siri ya ushindi huo ni kujituma na kufuata weledi, huku akisisitiza kwamba elimu aliyopata leo itamsaidia kufanya biashara kwa weledi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live