Serikali imesema haitovumilia kuona vitendo vya ukatili hasa Ukeketaji vinaendelea kufanywa katika jamii kwani vinasababisha madhara makubwa kwa watoto wa kike na wanawake.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akiwa wilayani Serengeti, mkoa wa Mara alipotembelea kituo cha Hope for Girls and Women kuona shughuli zinazofanywa na kituo hicho katika kupambana na ukeketaji.
Mpanju ameongeza kuwa Wizara itashirikiana na Wizara za kisekta na wadau ili kuhakikisha mapambano dhidi ya vitendo vya Ukeketaji yanaenda kwa kasi zaidi kwa lengo la kutokomeza vitendo hivyo katika Mikoa mbalimbali.
Aidha ameitaka jamii na wadau kuwalinda Watoto wa kike na wanawake dhidi ya vitendo vya Ukeketaji na kusisitiza kuwa hakuna Jamii ambayo inaruhusu kukatiza ndoto na maisha ya watoto wa kike kwa kuwafanyia vitendo vya Ukeketaji.
"Tunaweza kuishi katika jamii ambayo haina vitendo vya Ukeketaji katika maeneo yenu tuwalinde Watoto wetu wa kike kwani ni Hazina na tegemeo kwa maendeleo ya Taifa" alisema Mpanju
Pia amewataka Viongozi wa Kimila kuachana na Mila zilizopita kwa wakati ili kuwaokoa Watoto wa kike na vitendo vya Ukeketaji ambavyo vinasababisha Watoto wengi kupoteza ndoto zao katika maisha.
Akitoa taarifa ya Wilaya Afisa Maendeleo ya Jamii Wa Wilaya ya Serengeti Sunday Wambura amesema Wilaya inashirikiana na wadau Wilayani humo katika kutoa elimu kwa wananchi hasa mangariba na Wazee wa Kimila ili waweze kuachana na vitendo hivyo ambavyo vinasababisha hofu, vifo na matatizo ya kisaikolojia kwa watoto wa kike na wanawake.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Hope for Girls and Women Robi Samwel amesema Kituo hicho kimelenga kimewasaidia Watoto wanaokimbia kukeketwa kwa kuwapa hifadhi na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuachana na vitendo vya ukatili hasa vitendo vya Ukeketaji kwa kuwawezesha mangariba walioacha kukeketwa kupata fursa za kujikwamua kiuchumi na kuachana na vitendo hivyo.
"Pia tunawaendeleza wahanga wa Ukeketaji na waliokimbia vitendo hivyo kwa kuwawezesha kupata ujuzi katika fani mbalimbali ili waweze kujitegemea katika kuendesha maisha yao na wengi wamefika katika hatua za juu akiwemo mmoja aliyepo Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam" alisema Robi.