Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yapongezwa uimarishaji mikopo kwa vijana

A118c663ab1d748430eab3f1b901e6a6 Serikali yapongezwa uimarishaji mikopo kwa vijana

Wed, 31 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TAASISI ya Shirikisho la Vijana viongozi nchini,Youth Partnership Countrywide (YPC) imeipongeza Serikali kwa kuendelea kufanyia maboresho sera ya vijana ikiwemo Sera ya vijana ya namna ya kupata mikopo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika kongamano la vijana viongozi jijini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya vijana ya (YPC), Israel Irunde alisema sera ya vijana kwa sasa inaruhusu kukopesha kuanzia vijana watano na si kumi kama ilivyokuwa awali.

"Tangu mwaka juzi na mwaka jana tulizungumza sana kuwasaidia vijana kwanini vijana wapewe mikopo wakiwa 10 wakati hawafahamiani, kwanini watu wenye ulemavu walazimishwe kukaa kwenye kikundi cha watu 10 wakati ni vigumu kuwakutanisha hata wawili lakini hivi karibuni Waziri Jafo wa TAMISEMI tayari alishatangaza kanuni zilishabadilishwa sasa vijana wanaweza kupata mikopo hata wakiwa watano na watu wenye ulemavu anaweza kupata mikopo serikalini hata akiwa mmoja"alisema.

Mkurungenzi huyo alisema inapigania kuhakikisha vijana wanapata kazi zenye staha wakiwa wanaajiriwa au wamejiajiri wenyewe na kwamba vijana wasitumiwe kama ndala.

Mratibu wa YPC, Fred Mtei alibainisha lengo la kongamano hilo ni pamoja na kuangalia namna ya kutatua changamoto za vijana huku Irine Ringo akisema moja ya manufaa ya kongamano hilo ni kujiamini kwa vijana .

Mkurugenzi kutoka Taasisi ya Maendeleo ya vijana ya Open Mind Tanzania, Wakili, Dominick Nduguru akiwasilisha mada yake alisema kuna uhitaji wa sera bora ya vijana pamoja na watu wenye ulemavu kuhusishwa zaidi juu ya mapitio ya sera ya vijana.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kazi,Vijana ,ajira na wenye ulemavu, Amina Sanga aliwataka vijana kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali kwa vijana ikiwemo mafunzo ya kujitolea ya kuwajengea uwezo namna nzuri ya kuchangamana na watu mbalimbali ili kupata fursa zinazoweza kujitokeza ikiwemo kubadilishana ujuzi na uzoefu.

Taasisi ya vijana ya YPC ilisajiliwa mwaka 2003 kama kampuni isiyopata faida chini ya sheria ya makampuni na mwaka 2019 ilisajiliwa kama asasi ya Kiraia (NGO) ikiwa na lengo wa kujenga uwezo kwa vijana jinsia zote ambapo katika kongamano hilo vijana kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania wamekutana kujengewa uwezo ikiwa ni pamoja na namna ya vijana kufikia fursa .

Chanzo: www.habarileo.co.tz