Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema Serikali imeongeza zaidi ya Sh28.7 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kupitia mpango wa Maendeleo ya Taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19 katika Mkoa huo.
Amesema hayo leo Novemba Mosi ,2021 na kusema kwamba fedha hizo zitaelekezwa kwenye miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 464 ambavyo vitagharimu Sh9.3 bilioni huku kiasi cha Sh2.3 zikizotokana na tozo za simu zitatumika katika ujenzi wa vituo vya afya saba na vyumba vya madarasa 14.
Homera ametaja miradi mingine iliyopewa kipaumbele kuwa ni ujenzi wa jengo la huduma za dharura, mabweni, majengo matatu ya huduma za mashine za X-ray , nyumba za watumishi 6 zenye thamani ya Sh540 zitakazojengwa katika halmshauri za Busokelo, Chunya, Mbarali, Kyela, Rungwe na Wilaya ya Mbeya.
"Katika mgawanyo wa fedha hizo huduma ya dharura zimetolewa Sh 1.7 bilioni pamoja na vifaa, mabweni mawili Sh160 Milioni katika halmashauri za Busokelo na Rungwe ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mashine za x-ray tatu zenye thamani ya Sh1.3 bilioni" amesema.
Amesema kuwa upande wa miradi ya maendeleo kwa bajeti ya mwaka 2021/22 zimetengwa jumla ya Sh9.1 Bilioni kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kuboresha miundombinu ya majengo katika katika halmashauri za Busokelo, Chunya na Mbeya.
"Pia Sh 606.6 milioni kitatumika katika ujenzi wa vyumba vya madarasa 30 katika shule za msingi na shule maalumu , mahabara mbili zitakazogharimu Sh 300 milioni katika halmashauri za Chunya na Rungwe .
Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya mabadiliko makubwa katika katika Mkoa wa Mbeya hususan sekta ya elimu hivyo kuna sababu jamii kuhamasishwa kuchangia nguvu kazi.
Mkazi wa Iganzo jijini hapa, Faustina Sanga alipongeza utendaji na uwazi wa Rais Samia Suluhu kwani unaleta msukumu kwa jamii kushiriki na kuchangia shughuli za miradi ya Maendeleo hususan ujenzi wa miradi ya miundombinu ya vyumba vya madarasa ,sekta ya afya.