Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaombwa kuingilia kati mgogoro Kilombero

Image 178 1080x640.png Serikali yaombwa kuingilia kati mgogoro Kilombero

Tue, 13 Dec 2022 Chanzo: Dar24

Serikali imeombwa kuingilia kati mgogoro wa ardhi unaopelekea Wananchi kukimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wao, unaoendelea katika kijiji cha Merela kata ya chita halmashauri ya Mlimba wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

Mgogoro huo, unadaiwa kumuhusisha mwekezaji mtanzania na wananchi juu ya eneo lililopo katika kijiji hicho lenye ukubwa zaidi ya Hekari 2000 wakidai muhusika hana uhalali wa kumiliki kwani wao wameishi hapo kwa zaidi ya miaka 20 wakiwa wanaendelea na shughuli zao za kilimo na ufugaji.

Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho amesema, wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kikatili ikiwemo baadhi ya wanawake kuingiliwa kimwili bila ridhaa yao na wanaodaiwa ni maofisa wa Polisi ili kuondoka eneo hilo, jambo ambalo limezua taharuki na jamii kukimbia makazi yao.

Amesema, “kuna familia ya wakazi zaidi ya 1000, mpaka sasa hivi tunaomba serikali itusaidie kwa hili, hatulali ndani, wake zetu wanalala nyumbani mara nyingine wanabakwa, hatuna msaada kwenye ofisi ya kijiji, wilayani mpaka mkoani.”

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho, wanadai kuwa walifungua kesi ya kupinga mwekezaji huyo kuendelea kutumia eneo hilo, sintofahamu iliibuka baada ya miezi kadhaa mwekezaji huyo kurudi kijijini hapo nakudai kuwa mahakama imeshatoa hukumu kuwa yeye yupo kisheria kumiliki eneo hilo, jambo ambalo wananchi hao wadai kuwa kesi bado inaendelea na hukumu haijatolewa.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa kijiji cha Merela Hashimu Ngwembe alisema Serikali ya kijiji hicho haitambui mgogoro huo, kwa sababu mahakama ilishatoa hukumu kwa kumuagiza mwekezaji aendelee na shughuli zake katika eneo lenye Hekari 2000 kwenye kitongoji cha Msondo.

“Serikali ya kijiji hatuna mgogoro na mwekezaji tunaamini mwekezaji yupo kisheria, ndio maana hata kwenye mahakama zilizozungumzwa hizi kesi hukumu zake zilitoka kuwa mwekezaji aendelee na shughuli zake, pia wananchi, mwekezaji na serikali ya kijiji tulishakubalina ila kuna baadhi ya watu wachache ambao wao wanaona bado wanahaki ya kuendelea kuwa sehemu hiyo ya mwekezaji” alisema kaimu mwenyekiti Ngwembe

Hata hivyo, Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro Fortunatus Muslimu amesema jeshi la Polisi linafanya doria za kawaida kutafuta wahalifu na sio kuondoa wananchi kwenye maeneo hayo.

Chanzo: Dar24