Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yamkana Hapi kuhusu vitambulisho

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mwita Waitara amesema maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi kuhusu makundi yanayotakiwa kupewa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo si ya Serikali.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Mei 31 2019 bungeni Jijini Dodoma na Waitara baada ya wabunge kupitisha bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi 2019/2020. 

Waitara amesema katika kikao cha  Rais John Magufuli, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wakuu wa mikoa wa Tanzania Bara, alitoa vitambulisho 650,000 kwa wakuu wote wa mikoa kwa awamu ya kwanza.

Amesema kwa awamu ya pili, alitoa vitambulisho milioni 1.2 na hivyo kufanya jumla ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa kufikia milioni 1.85.

Waitara amesema  ili kupata vitambulisho hivyo, wafanyabiashara na watoa huduma wadogo wanatakiwa kulipa Sh20,000 kwa kitambulisho kimoja.

Amesema lengo la Serikali ni kuwatambua wafanyabiashara wadogo na watoa huduma wadogo ambao mauzo ghafi yao hayazidi Sh4milioni kwa mwaka.

Pia Soma

Amezitaja sifa za mfanyabiashara anayetakiwa kupewa kitambulisho awe na mapato ghafi yasiyozidi Sh4milioni kwa mwaka, awe hajawahi kuandikishwa na kupewa namba ya kitambulisho cha mlipa kodi (TIN).

Pia awe anatambulika kama mfanyabiashara ama mtoa huduma mdogo kupitia ofisi ya mtendaji wa mtaa ama kijiji kwa mujibu wa sheria.

Amesema hadi kufikia Mei 26, jumla ya vitambulisho milioni 1.85 vimegawiwa kwa wakuu wote wa mikoa Tanzania Bara.

Waitara amesema vitambulisho 1,176,305 vimegawiwa kwa wafanyabiashara na watoa huduma wadogo na tayari Sh23.5 bilioni zimekusanywa.

Amesema ili kuboresha kazi hiyo, Serikali imekamilisha mwongozo wa ugawaji wa vitambulisho hivyo na utaanza kutumika mwaka wa fedha 2019/2020.

“Tamko linaloendelea kuzunguka katika mitandao ya jamii na vyombo vya habari likimhusisha mkuu wa mkoa wa Iringa sio maelekezo ya Serikali.

“Hivyo ninatoa wito kwa wakuu wote wa mikoa, watendaji wote kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na serikali kuhusu ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara na watoa huduma wadogo,” amesema.

Mwisho

Chanzo: mwananchi.co.tz