Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeumaliza mgogoro wa matumizi ya ardhi wilaya Mbarali mkoani Mbeya uliodumu kwa miaka 15 ambao ulihusisha wakazi wa wilaya hiyo katika eneo la Bonde la Usangu dhidi ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Akizungumza katika kikao na wadau waliowekeza katika Bonde la Usangu wakiwemo wakulima wa mashamba ya mpunga, mashine za kukoboa mpunga na wafugaji katika vitalu kilichofanyika jana (Januari 16, 2023) mkoani Mbeya, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanya maboresho makubwa kwenye Tangazo la Serikali namba 28 ambayo itawawezesha wananchi kufanya shughuli za kilimo na ufugaji endelevu.
Amesema marekebisho ya tangazo hilo yatawezesha baadhi ya vitongoji vilivyokuwa vimetangazwa awali kuwa ndani ya hifadhi kuachwa nje ya mipaka ikiwemo kutoa eneo la hekta 74,000 kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.
“Hii GN 28 Serikali tumeamua kuitafutia ufumbuzi baada ya vikao vingi na wadau kwa faraja kabisa nataka niwaambie tumefikia hatua nzuri itakayowezesha kila anayejishughulisha na kilimo kuendelea na kilimo chake na kila anayejishughulisha na mifugo kuendelea na ufugaji yake.”
Amesema kuwa Serikali inataka kuhakikisha Wilaya ya Mbarali inaendesha shughuli za kilimo kitaalam na kwa tija. “Tumeona maendeleo makubwa na ujenzi wa viwanda vya mtu mmoja mmoja na vikundi, Serikali inataka kuona shughuli hizo zinakuwa endelevu, tunataka mpanue viwanda vyenu na mzalishe zaidi.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeamua kuitoa nje ya hifadhi ranchi ya Usangu kwa ajili ya shughuli za ufugaji wa kisasa. “GN namba 28 iliingiza ranchi ndani ya hifadhi, lakini ili wafugaji wawe huru tumeindoa na hivyo itakuwa nje, tumeacha na mito kadhaa ambayo itahifadhiwa kwa sheria za mazingira.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wafugaji kujiamini kwani mifugo ni uchumi. “Tunataka tuondokane na uchungaji na kuwafanya Watanzania wafugaji kuacha kutembea umbali mrefu na ng'ombe kwani inaondoa thamani ya nyama, tunataka mfuge kisasa.”
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula amesema kuwa maeneo ambayo yameondolewa katika hifadhi watahakikisha mpango bora wa matumizi ya ardhi unawekwa ili wananchi waweze kufanya kile ambacho kimepangwa kufanyika kwa wakati huo.
Ameongeza kuwa watahakikisha wananchi hao wanapata hati miliki za maeneo yao ili waweze kuzitumia katika shughuli mbalimbali za maendeleo na mpango wa uandaaji utafanyika kwenye vijiji vyote vinavyohusika.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo amesema kuwa kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji watumiaji wote wanapaswa kuheshimu sheria ya mazingira.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana amewataka watumiaji wa eneo lililotolewa kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kilimo waendelee kulilinda eneo lililobaki. “Tusifuge wala kulima katika eneo lililobaki eneo hili ni chanzo kikubwa cha maji na sehemu ya utalii”.
Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema ranchi ya Usangu ni kwa ajili ya shughuli za ufugaji tu na isitokee yeyote akafanya tofauti na lengo. “Tulioko kwenye ranchi tufuge, wengine mnabadilisha matumizi wengine hamfugi lakini mnakodisha watu wanakuja kulima kwenye vitalu, wale mnaolima badala ya kufuga tutawanyang’anya vitalu.”