Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yakamilisha mradi wa maji Chalinze

Maji Pic Data Serikali yakamilisha mradi wa maji Chalinze

Sun, 7 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Adha ya maji katika mji wa Chalinze mkoani Pwani imepatiwa ufumbuzi wa kudumu baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa Mlandizi- Chalinze-Mboga utakaozalisha lita milioni tisa kwa siku.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo na kuwasha valvu ya kuruhusu maji kuanza kutoka Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema wizara yake inafanya kila jitihada kuhakikisha changamoto ya maji katika maeneo mbalimbali inakuwa historia.

Kuhusu mradi huo Aweso amesema umetekelezwa kwa fedha za ndani zilizotolewa na Serikali huku msukumo mkubwa ukitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Mradi uliasisiwa na Rais wa awamu ya tano hayati John Magufuli, lakini mama alivyokuja hakusita kuhakikisha unaendelea kutekelezwa na kukamilika ili kuwaondolea adha wakazi wa Chalinze, leo umekamilika na tatizo la maji linakwenda kuwa historia.

“Wito wangu kwa mamlaka nyingine za maji kusimama kikamilifu kuhakikisha miradi yote iliyoanza kutekelezwa kukamilika kama ambavyo Dawasa wamefanya katika mradi huu,”amesema Aweso.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya Sh18 bilioni ukihusisha ujenzi wa kituo cha kusukuma maji.

Sambamba na kituo hicho chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni moja kwa siku umehusisha pia ulazaji wa bomba lenye urefu wa kilomita 59.5.

Luhemeja amesema mradi utazalisha maji lita milioni tisa kwa siku kiasi ambacho kitamaliza adha ya maji kwa wakazi wa mji wa Chalinze.

“Mahitaji ya maji kwa mji wa Chalinze ni lita milioni 12 kwa siku, ambapo mtambo wa Wami unazalisha maji lita milioni 6.8 kwa siku, hivyo maji ya mradi wa Mboga pamoja na ya kutoka Wami yatatosha kabisa kuhudumia mji wa Chalinze kwa miaka miwili ijayo,”.

Chanzo: mwananchidigital