HATIMAYE serikali imekabidhi hati miliki kwa wakazi 644 wa Magomeni Kota, Dar es Salaam na kuwaeleza kuwa watahamia rasmi kwenye nyumba hizo mwezi ujao.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe wakati akikabidhi hatimiliki za nyumba hizo kwa viongozi wa wakazi hao na kuwaeleza kuwa azma ya serikali ni kuona wanaishi kwenye makazi bora waliyoahidiwa awali.
“Serikali kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imehakiki wahusika halali wa wanaopaswa kuishi kwenye hizi nyumba na tumewabaini wote na leo tumetoa hati miliki kwa wakazi 644 kupitia chama chenu na mtaingia kwenye nyumba kuanzia mwezi ujao, taratibu nyingine zinaendelea za jinsi ya kukaa hapa,” alisema Gondwe.
Mtendaji Mkuu wa TBA, Daud Kondoro alisema ujenzi wa mradi huo umekamikika kwa asilimia kubwa na kilichobaki ni kufungwa kwa lifti ndani ya majengo hayo na kueleza kuwa muda wowote kuanzia sasa kazi hiyo itakamilika.
“Wakazi 98 waliokuwa wapangaji hapa majina yao yalileta mkanganyiko na majina tuliyokuwa nayo kwenye mikataba ya upangaji ambayo iko kwenye mafaili yetu, hata hivyo nyumba tisa zimepangishwa Ofisi ya Rais na nyumba 44 wataishi mtu zaidi ya mmoja kwa wale warithi ambao walirithi ndugu zao wamefariki,” alisema Kandoro Alisema katika tathmini yao wamebaini wakazi saba waliokuwa wapangaji wa awali kwenye nyumba hizo hawajulikani walipo na juhudi za kuwapata zimeshindikana