Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yafuta mapori 12 Dodoma, vijiji 40 vyabaki  

A73d8c945172427ad05349928dd43910.jpeg Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi

Thu, 7 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imefuta mapori 12 mkoani Dodoma lakini imevibakisha vijiji 40 kati ya 42 ambavyo wananchi walikuwa wakiishi na kuendesha shughuli zao kwenye maeneo ya hifadhi na mapori ya akiba.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema mapori yaliyofutwa yana ukubwa wa ekari 707, 659 na pia ekari 46,755 za misitu 12 zimefutwa kwa ajili ya kuwamegea wananchi sehemu ya maeneo hayo ili wayatumie kwa shughuli za uzalishaji.

“Vijiji vyote 40 katika mkoa huu wa Dodoma vitabaki ila ndani ya vijiji 20 kuna vitongoji tutavifanyia tathmini upya na suala hili litakuwa shirikishi,” alisema Lukuvi alipozungumza na wananchi wa vijiji vya Bubutole na Mwombose wilayani Chemba katika Mkoa wa Dodoma.

Lukuvi ni kiongozi wa kamati ya mawaziri wanane waliopo kwenye ziara ya kutoa mrejesho wa ufumbuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo ya hifadhi na mapori ya akiba.

Alisema tayari Tangazo la Serikali (GN) za misitu na mapori ya akiba vilivyokuwemo vijiji hivyo imefutwa na sasa taasisi zenye dhamana na maeneo ya hifadhi zinatakiwa kulinda na kuweka alama za mipaka kwenye maeneo yaliyobaki ili yasivamiwe.

Lukuvi alisema vijiji viwili kati ya 42 katika mkoa huo wa Dodoma itabidi viondolewe kupisha ujenzi wa Bwawa la Maji la Farkwa katika Wilaya ya Chemba alivitaja kuwa ni Bubutole na Mwombose wilayani humo.

“Serikali tayari imelipa fidia kwa wananchi katika vijiji hivi na wale ambao fidia haikwenda vizuri serikali ipo na kila mtu lazima alipwe kulingana na mali zake na na Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu ameshatoa fedha kwa ajili ya huduma za shule, zahanati pamoja na maji pale mtakapokwenda,” alisema.

Wakazi 2,829 kati ya 2,868 sawa na asilimia 99 katika vijiji hivyo viwili wamelipwa fidia.

Bwawa la Farkwa litakuwa na ukubwa wa kilometa za mraba 68 na mita za ujazo milioni 470 na litanufaisha wakazi wa Jiji la Dodoma, wilaya za Chemba, Bahi, na Chamwino na vijiji vyote vitakavyopitiwa na bomba hilo.

Agosti 7, mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 ipatiwe ufumbuzi bila kuleta taharuki kwa kuzingatia maslahi ya taifa. Agizo hilo limeanza kutekelezwa kwenye vijiji 920.

Chanzo: www.habarileo.co.tz