Mwanza. Serikali imepiga marufuka kazi ya kuchimba udongo wa kutengeneza majiko ya mkaa katika eneo la milima ya Mabumbani mtaa wa Tambukareli jijini Mwanza baada ya mchimbaji mmoja, Ndawala Ndobo kufariki dunia kwa kufukiwa na udongo na kuangukiwa na miamba.
Amri ya kufunga machimbo hayo imetolewa leo Machi 28, 2019 na Mkuu wa Wilaya ya Nyamaghana, Dk Philis Nyimbi baada ya mwili wa mchimbaji huyo kupatikana kufuatia kazi ya uokoaji iliyochukua siku tatu tangu Machi 25, 2019.
“Kwa siku tatu tuliyofanya kazi ya kutafuta mwili wa mwenzetu (marehemu Ndobo), tumejiridhisha kuwa eneo hili ni hatarishi kwa kwa usalama na maisha ya watu na nimepiga marufuku kazi ya kuchimba udongo eneo hilo kuanzia leo,” amesema Dk Nyimbi.
Amesema njia walizokuwa wakitumia wachimba udongo kwenye milima hiyo zinapita chini na katikati ya mawe makubwa zinazoweza kuwaangukia watu.
“Atakayekaidi amri hii halali atakumbana na mikono ya dola kwa kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria,” alisisitiza mkuu huyo wa wilaya.
Akizungumzia matukio ya watu kupoteza maisha eneo hilo, mmoja wa wachimba udongo, Ashura Khamisi amesema kifo cha Ndobo kimefikisha idadi ya watu watano tangu mwaka 2000 alipoanza kazi hiyo.
Akishukuru kwa niaba ya familia, John Ndobo ambaye ni kaka wa marehemu ameishukuru Serikali kwa kufanikisha mwili wa ndugu yake kupatikana na kuzikwa kwa heshima.
“Pia tunashukuru kwa rambirambi ya Sh200, 000 iliyotolewa na mkuu wa wilaya ambayo tutafanikisha mazishi ya heshima ya ndugu yetu,” amesema John.
Mazishi ya Ndogo yanatarajiwa kufanyika leo katika makaburi ya Tambukareli eneo Mahina jijini Mwanza.