Serikali imesema uthamini wa makazi ya wananchi waliopisha Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi, haukuhusisha ardhi bali mali zisizohamishika.
Kauli hiyo ya Serikali imekuja muda mchache baada ya malalamiko ya wananchi hao kuhusu viwango vya fidia visivyolingana na thamani halisi ya makazi yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Machi 10, 2023 kuhusu uthaminishaji huo, Mratibu wa Miradi ya Serikali inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, Mhandisi Humphrey Kanyenye amesema viwango vya fidia vimetokana na uhalisia wa mali zisizohamishika zilizokutwa wakati wa uthamini.
"Kilichofanyiwa uthamini ni kile kilichokutwa kwenye eneo husika, wengi walikuwa na matarajio makubwa lakini hatukuhusisha ardhi tumeangalia kile tulichokikuta kwenye eneo husika," amesema. Amesema uthamini huo haukuhusisha ardhi kwa sababu eneo hilo lilishatolewa notisi na Serikali mwaka 1979 kwamba halipaswi kuendelezwa na yeyote.
Wananchi Akizungumza na Mwananchi Digital, mmoja wa wananchi, Teresia Thadei amesema anashangaa nyumba yake yenye vyumba viwili anatakiwa kulipwa Sh1.2 milioni.
"Sasa nikilipwa kiasi hicho cha fedha nitafanya nini maana haitoshi hata kununua hata kiwanja mjini," amesema. Matilda Kalumba amesema nyumba yake yenye ukubwa wa vyumba 12 anatakiwa kulipwa fidia ya Sh4 milioni kiasi ambacho amedai ni kidogo kulingana na thamani halisi ya nyumba hiyo.