Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaeleza chanzo maji kutotosha Dodoma

Thu, 26 Nov 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Katibu mkuu wa Wizara ya Maji, Anthony Sanga amesema upungufu wa maji jijini hapa unatokana na ongezeko kubwa la watu kulinganisha na uzalishaji wa huduma hiyo.

Sanga alisema hayo jana baada ya Rais John Magufuli kulihutubia Bunge la 12 na kuzungumzia jinsi Serikali ilivyojipanga kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema mahitaji ya maji Dodoma ni lita milioni 102 huku kiwango kinachozalishwa kikiwa ni lita kati ya milioni 60 na 70 ambazo hazikidhi mahitaji ya watumiaji.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa Dodoma wamekuwa wakilalamikia tatizo la kukatika kwa maji huku wengine wakisema hawapati maji kwa muda wa siku saba mfululizo.

Katibu mkuu huyo alisema changamoto ya kiwango cha maji kinachozalishwa ambacho hakikidhi mahitaji kimesababishwa na ongezeko la watu jijini hapa.

“Dodoma imekuwa na ongezeko kubwa la watu, ndio maana kuna mahitaji ya maji lita milioni 102 wakati zinazozalishwa ni kati ya lita milioni 60 hadi 70,” alisema.

Pia Soma

Advertisement
“Kwa hiyo kuna gap kubwa. Tuwahakikishie Watanzania waliopo Dodoma kuwa upo mpango mkubwa wa kujenga miradi ya maji kutoka Ziwa Victoria na mradi wa Farkwa.”

Alisema miradi hiyo ikikamilika itakuwa ni mwarobaini wa changamoto ya uhaba huo.

Pia, alisema Serikali ilijenga miradi 1,422 ya maji kuhakikisha tatizo hilo linaisha, bado halijaisha hasa maeneo ya vijiji, hivyo imedhamiria kuhakikisha wananchi wote wanapata majisafi na salama.

Kwa mujibu wa tovuti ya Wizara ya Maji, Serikali ilitenga Sh7.7 bilioni ili kuwalipa fidia wananchi 2,868 wa vijiji vya Mombose na Bubutole wilaya ya Chemba, kwa lengo la kupisha ujenzi wa bwawa la maji la mradi wa Farkwa.

Mbunge wa Pangani aliyekuwa Naibu Wizara Maji, Jumaa Aweso alisema Tanzania kuna vyanzo vingi vya maji ila changamoto ni namna ya kujenga miundombinu.

Chanzo: mwananchi.co.tz