Dodoma. Serikali ya Tanzania imeelekeza halmashauri zote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya kuchimba mabwawa ya kufugia samaki na kuendeleza ufugaji wa samaki kwenye vizimba.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Juni 10, 2019 bungeni na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Mwita Waitara ambaye amesema jitihada nyingine ni kuwasaidia wavuvi nchini wakiwemo vijana na wanawake ikiwemo kuondoa kodi katika zana na malighafi.
Alikuwa akijibu swali la msingi la mbunge wa Viti Maalum (CCM) Janeth Massaburi ambaye ameuliza Serikali ina mpango gani kuwawezesha vijana na akina mama kwenye kila halmashauri nchini kutenga maeneo maalum ya kujenga mabwawa ya kufugia samaki ili makundi hayo yaweze kujiajiri.
Akijibu Naibu Waziri Mwita amesema Serikali imepunguza kwa sehemu kubwa mzigo wa gharama ikiwemo kufuta kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye injini za kupachika nyuzi za kushonea nyavu na vifungashio ambapo Serikali inalipia asilimia 40 na mvuvi anachangia asilimia 60 tu.
Amesema halmashauri zote nchini zimekuwa zikitoa mafunzo ya uvuvi endelevu kwa vijana na akina mama kupitia semina, warsha, vipeperushi, makala, redio na luninga kwa kushirikiana na wizara ya mifugo na uvuvi.