Dodoma. Serikali ya Tanzania imeunda kamati maalumu ambayo inatembea nchini kuhakikisha migogoro ya wafugaji na wakulima inapatiwa ufumbuzi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega leo Jumanne Aprili 30, 2019 akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi.
Shangazi amesema katika eneo la wafugaji la Mkundi tarafa ya Umba, kuna migogoro mara kadhaa.
“Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha sekta nzima ya ufugaji,” amehoji Shangazi.
Akijibu swali hilo, Ulega amesema Serikali imejipanga katika kutatua na kwamba wameunda kamati inayotembea nchi nzima kuhakikisha migogoro ya wafugaji inapatiwa ufumbuzi.
“Napenda kumhakikishia wizara inayo mipango mizuri ya kuhakikisha fursa zinapatikana… majosho yamechukuliwa (Serikali) na yako katika mpango kuhakikisha yanaboreshwa na yakikamilika tutakuja kuzindua,” amesema.
Mbunge wa Chambani (CUF), Salim Yusuf Hussein amehoji ni wapi kuna mfano wa eneo ambalo lina ufugaji bora na kilimo bora ambako watu wanaweza kwenda kujifunza.
Akijibu, Ulega amesema maeneo yapo mengi ya kujifunza na kutoa mfano wa Morogoro ambako kuna mfugaji mmoja anamiliki ng’ombe wa kisasa 700.
Naye Mbunge wa Monduli (CCM), Julius Kalanga amehoji iwapo kuna mkakati wa upatikanaji wa mbegu bora ili kusaidia wafugaji.
Akijibu swali hilo, Ulega amesema Serikali ina mpango kabambe wa kuhakikisha wanaboresha kwa kusimamia mifugo na uvuvi.
Amesema Serikali ina mikakati mitatu ikiwemo ule wa kupitia madume bora yanayopatikana katika mashamba yao.