Hai. Serikali ya Tanzania imeagiza kufutwa kwa hati ya kampuni ya mafuta ya Oryx iliyopo ndani eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Imesema eneo hilo lilichukuliwa kiujanja, kwamba haiwezekani kampuni hiyo kuwa na hati katika eneo ambalo tayari lina hati.
Agizo hilo limetolewa leo Jumamosi Julai 6, 2019 na naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wa Tanzania, Atashasta Nditiye wakati akikagua maeneo yenye mgogoro katika uwanja huo.
Ameitaka kampuni ya uendeshaji wa uwanja huo ya Kadco kutekeleza agizo hilo mara moja.
"Nimeongea na watu wa Kadco kufuta hati inayomilikiwa na Oryx. Ni jambo la kushangaza kuwa na hati ndani ya eneo lenye hati, nimeshangazwa na kusikitishwa si kitu cha kawaida.”
"Hawa Oryx wana hati ya kumiliki hili eneo katikati ya uwanja wa ndege ni kitu cha ajabu sana, iweje wamiliki hati ndani ya hati nyingine. Naomba hii hati ifutwe tunawapenda wawekezaji na tunawahitaji lakini tunataka walipe kodi kama wapangaji wengine wasimiliki ardhi kijanja,” amesema Nditiye.
Pia Soma
- Viongozi wawili Chadema wadaiwa watekwa
- Makubaliano ya Rais Magufuli, Kenyatta haya hapa
- Lugola awashukia polisi wanaowadhulumu wananchi ardhi